Imeelezwa kuwa baada ya msanii Elizabeth Michael kusomewa hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela, aliwaambia ndugu zake wasikate rufaa kwa kuwa kilichotokea ni mipango ya Mungu na yupo tayari kukabiliana nayo.
Msanii , Muhsin Awadh maarufu Dk Cheni ambaye amekuwa karibu na mwigizaji huyo katika kipindi chote amesimulia hali ilivyokuwa muda mfupi baada ya jaji kutoa hukumu hiyo.
“Kusema ukweli Lulu alijua lolote linaweza kutokea ila la kufungwa ni kama hakulipa kipaumbele sana, jaji alipomaliza kusoma hukumu alishtuka kama sisi wengine wote lakini ajabu alikuwa wa kwanza kurudi katika hali ya kawaida na kutoa kauli za ujasiri,” anasimulia Dk Cheni
Lulu alisema: "Sipingani na maamuzi ya Mungu, haya ni maamuzi yake na nimekubaliana nayo. Ana makusudi yake kunipa hiki kilichotokea leo".
Anasema kingine alichowaambia ni kuachana na masuala ya kukata rufaa kwa sababu bado hatakuwa huru: "Acheni miaka miwili siyo mingi, sitaki kupingana na mahakama , naheshimu maamuzi ya mahakama, acheni nitumikie kifungo changu. "
Mapema wiki hii mwigizaji huyo alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake Steven Kanumba, Aprili 7,2012.
No comments:
Post a Comment