Tshishimbi, Kamusoko wamtia hofu Lwandamina. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Friday 29 September 2017

Tshishimbi, Kamusoko wamtia hofu Lwandamina.

Inachopiga hesabu Yanga ni kuwavaa Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi kesho.
Tayari ina uhakika wa kumkosa kiungo wake, Mkongo, Pappy Kabamba Tshishimbi ambaye ana kadi tatu za njano lakini sasa imeingia katika hofu ya kumkosa kiungo wake tegemeo, Thabani Kamusoko baada ya Mzimbabwe huyo kupata dhoruba ndogo katika mazoezi ya jana.

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina raia wa Zambia, naye ameona ni vizuri kujipanga mapema, na tayari ameishachukua hatua.

Yanga wanatarajiwa kuvaana na Mtibwa Sugar, kesho Jumamosi kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Tshishimbi ndiye mchezaji wa kwanza kuondolewa kwenye mipango ya kocha wa timu hiyo, baada ya kupewa kadi ya tatu ya njano kwenye mechi iliyopita ya ligi kuu dhidi ya Ndanda FC iliyomalizika kwa timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0.

Kamusoko naye anatarajiwa kuukosa mchezo huo baada ya kupata majeraha ya goti na kutoka nje kwenye mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kamusoko akiwa nje anapatiwa matibabu, alimuomba daktari wa timu hiyo, Edward Bavu apumzike asiendelee na mazoezi kutokana na maumivu aliyokuwa anayasikia.

Mara baada ya Kamusoko kutoka, Lwandamina haraka akafanya maamuzi kwa kuwaandaa vijana wake wawili, Juma Makapu na kinda Maka Edward aliyepandishwa kikosi cha kwanza katika msimu huu wa ligi kuu ili wacheze namba sita inayochezwa na Tshishimbi ambaye ataukosa mchezo huo kutokana na adhabu hiyo ya kadi tatu za njano.

Lwandamina alionekana kuwandaa wachezaji hao kucheza namba sita baada ya Kamusoko aliyekuwa anatakiwa acheze namba sita mechi na Mtibwa kupata majeraha hayo na kulazimika kuwanoa vijana wake hao.

Wakati akiwaandaa wachezaji hao, katika mechi hiyo dhidi ya Mtibwa kocha huyo anatarajiwa kumtumia kiungo wake mpya, Pius Busitwa aliyekosa michezo minne ya ligi kuu kwa kukiuka kanuni za usajili kwa kusaini klabu mbili Simba na Yanga ambaye tatizo lake limemalizika.

Busitwa kwenye mechi hiyo, anatarajiwa kucheza namba nane iliyokuwa inachezwa na Kamusoko kwenye michezo iliyopita huku winga ya kushoto akianza kucheza Raphael Daudi.

Alipoulizwa Bavu kuzungumzia afya ya Kamusoko, alisema:
"Kamusoko amejitonesha goti lake aliloumia muda mrefu na kama ulivyoona ameshindwa kuendelea kwa ajili ya kumfanyia vipimo.

"Kikubwa kinachosababisha wachezaji wangu kujitonesha majeraha yao na wengine kupata majeraha mapya ni kutokana na hali ya uwanja ambao tunautumia, kiukweli ni mgumu lakini hatuna jinsi, inatubidi tuendelee kuutumia kwa sababu ndiyo uwanja tunaoutumia kuchezea mechi za ligi kuu," alisema Bavu.

No comments:

Post a Comment