Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema suala la Rais John Magufuli kusafiri nje ya nchi haliepukiki.
Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ya mwaka 2018/19 bungeni mjini Dodoma, Sugu amesema kuna mikutano inayopaswa kuhudhuriwa na rais mwenyewe, si kuwakilishwa na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Rais Magufuli amewahi kueleza kuhusu safari zake, kubainisha kuwa hakuchaguliwa na Watanzania ili kusafiri nje ya nchi.
Magufuli ametembelea Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia katika kipindi chote cha utawala wake huku akitimiza takribani miaka miwili na nusu tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.
Machi mwaka huu Rais Magufuli akiwa mjini Singida katika uzinduzi wa kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mount Meru Millers Group, alisema amekataa zaidi ya mialiko 70 ya kwenda nje ya nchi kwa sababu hakuchaguliwa na Watanzania kwenda huko bali kuwatumikia.
Amesema jimbo lake ni Tanzania na kwamba hawezi kwenda wakati hajamaliza kutatua kero za wananchi waliompigia kura na wabunge wa chama chake CCM.
“Suala la kusafiri bado ni muhimu, tena anapokwenda nje anaweza kutumia lugha ya Kiswahili kwa sababu Rais Xi Jinping wa China kila anapokwenda anaongea kichina licha ya kuwa msomi na anazungumza Kiingereza,” amesema Sugu.
“Kama tatizo ni gharama, mbona anatuma delegation (ujumbe) mara makamu wa rais, mara waziri mkuu nao wanatumia gharama kwa sababu hawaendi kule kwa miguu, sasa hatuendi UN (Umoja wa Mataifa), Davos, Commonwealth.”
Sugu ambaye hivi karibuni alitoka gerezani kwa msamaha wa Rais amesema, “mikutano ya common wealth (Jumuiya za Madola) ni ya wakuu wa nchi lakini sisi tunatuma wawakilishi, kuna fursa za kiuchumi na kibiashara.”
“Rais Uhuru Kenyatta (wa Kenya) ametumia vizuri sana fursa za uchumi na kibiashara kwa nchi yake alivyokwenda pale hali kadharika Rais wa Afrika Kusini nae anatumia fursa.”
Amesema kutokana na fursa hizo, rais kusafiri nje hakuepukiki, “ni kama alivyonukuliwa mzee Kikwete (Jakaya-Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne) aliposema kusafiri kumemsaidia sana kwani mkaa bure si sawa na mtembea bure.”
No comments:
Post a Comment