NI siku 20 sasa tangu aliyekuwa video queen maarufu Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ aage dunia. Bado taswira yake haiondoki kwenye macho na mawazo ya aliyekuwa mzazi mwenzake kabla ya kuachana, Sabri Shaban Othuman ambaye walijaliwa kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Sanie Sabri.
Risasi Vibes lilifanya makala maalum na Sabri ambaye ni mkazi wa Magomeni jijini Dar huku akifanyia biashara zake maeneo ya Tip-Top, Manzese. Katika mahojiano haya, Sabri ana mengi ya kumwelezea mzazi mwenzake, Masogange aliyekiri kuwa alikuwa zaidi ya mzazi mwenziye kutokana na walivyokuwa wameshibana, ungana naye;
Risasi vibes: Mashabiki wangependa kujua, wewe na Masogange mlikutana wapi?
Sabri: Tulikutana Magomeni, tulikuwa tunaishi mtaa mmoja.
Risasi vibes: Watu wamekuwa wakieleza kwamba eti Masogange alikuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwenu ndipo ukampa ujauzito, je, ni kweli?
Sabri: Hapana, siyo kweli, Masogange alikuwa anaishi kwa shangazi yake mtaa mmoja na ninapoishi mimi hadi sasa na ndipo tulipokutana hapo.
Risasi vibes: Mlianzisha uhusiano wa kimapenzi mwaka gani?
Sabri: Ni kwenye miaka ya 2002 au 2003. Tulipata mtoto mwaka 2006, wakati huo nilikuwa nikiishi naye nyumbani kwa mama yangu, Ilala (jijini Dar).
Risasi vibes: Je, mlifunga ndoa?
Sabri: Hatukuwahi kufunga ndoa, lakini tulikaa kwenye uhusiano kama miaka sita hivi ndipo tukaachana.
Risasi vibes: Nini kilichosababisha mkaachana?
Sabri: Hakuna sababu ya msingi ya kuachana. Nakumbuka nilisafiri, nilikwenda nje ya nchi ambako nilikaa kwa miaka miwili na nusu, hukohuko nikaanzisha uhusiano na mtu mwingine na niliporudi, nilimkuta Masogange naye ana uhusiano mwingine hivyo kila mmoja akaendelea na maisha yake huku tukiulizana mambo yanayomhusu mtoto ambaye alikuwa anaishi kwa dada yangu.
Risasi vibes: Kwa nini mliamua mtoto aishi kwa dada yako na siyo mama yake?
Sabri: Kutokana na kwamba tulimpata mtoto akili zetu zikiwa hazijapevuka vizuri kwani Masogange kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 19 na mimi nilikuwa na 20 hivyo, dada zangu waliona hatuwezi kumlea vizuri ndipo akamchukua.
Risasi vibes: Kuna habari kwamba mlikuwa mmemkataza Masogange asimwanike mwanaye kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, hili likoje?
Sabri: Ni kweli, nilikuwa namwambia asimweke mtoto kwenye vyombo vya habari maana siyo kitu kizuri na bado ni mdogo.
Risasi vibes: Masogange alikuwa mtu wa aina gani kwako?
Sabri: Masogange alikuwa ni zaidi ya mzazi mwenzangu, alikuwa rafiki yangu sana maana hata kabla ya kuingia naye kwenye uhusiano, tulikuwa marafiki mno hivyo hata baada ya kuachana, tulikuwa marafiki sana hata siku anaanza kuugua, alinipigia simu usiku na kuniambia anajisikia vibaya, nikamwambia aende hospitalini.
Risasi vibes: Ni kitu gani ambacho hutakisahau kwa Masogange?
Sabri: Vipo vingi sana, kwanza nammisi yeye mwenyewe na ucheshi wake. Pia jinsi tulivyokuwa tukishauriana mara kwa mara kwamba tumlee mtoto wetu vizuri hivyo nitaendeleza hayo kwa kumpa mtoto wetu malezi bora kabisa na kila anachokihitaji nitamtimizia kama mzazi ili nisimwangushe Masogange.
Risasi vibes: Vipi hali ya mtoto baada ya mama yake kufariki dunia?
Sabri: Kuna wakati anakosa raha kabisa, anajiinamia tu, anakuwa mpweke hivyo nikiona hivyo mimi na shangazi zake, tunakuwa na kazi ya kucheza naye michezo mbalimbali ili asahau, awe sawa.
Risasi vibes: Je, ana dalili zozote za kufuata nyendo za mama yake kwenye sanaa?
Sabri: Dalili anazo sana, nami siwezi kumkataza, anachokipenda nitamuunga mkono na kumwendeleza kipaji chake na kila akipendacho kilicho kizuri.
Risasi vibes: Tofauti na mtoto huyo, unaye mwingine na je, umeoa?
Sabri: Sina mtoto mwingine zaidi ya huyo. Pia bado sijaoa ila nina mpenzi na wakati wa kuoa bado, ukifika nitaoa tu.
Risasi vibes: Utamuenzi Masogange kwa kitu gani?
Sabri: Nitamuenzi kwa kumlea mwanangu vizuri na kumsapoti kwa kile anachokitaka maana Masogange tuliishi vizuri, hatukuachana kwa ugomvi, tulikuwa marafiki sana na tulikuwa tunazun-gumza vyema.
Risasi vibes: Nashukuru kwa ushirikiano wako kaka.
Sabri: Karibu sana
No comments:
Post a Comment