Klabu ya Yanga, imefunguka na kuwatoa hofu mashabiki wa wanajangwani kuwa kukosekana kwa nyota wao wanne katika kikosi kilichosafiri Mei 03, 2018 kuelekea Algeria kuwa hakiusiani na masuala ya mgomo wowote bali kimetokana na baadhi ya wachezaji hao kuwa majeruhi na majukumu ya kifamilia
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Dismas Ten baada ya kuzuka mjadala mkubwa kwa wapenzi wa soka nchini ambapo kila mmoja amekuwa akisema lake na wengi kuhusisha na suala ukosefu wa fedha ambalo linaonekana kuwa ni changamoto kubwa kwenye klabu hiyo kwa kipindi hiki.
"Taarifa ya awali za benchi la ufundi na taratibu za safari zilikuwa zimeshafanyika kwa wachezaji wote akiwemo Ibrahi Ajib, Kelvin Yondan, Papy Kabamba pamoja na Obrey Chirwa nikiwa na maana walikuwa katika kikosi kinachotakiwa kusafiri kuelekea Algeria lakini kuna mambo yakajitokeza ya kibinaadamu ndio yakasababisha kutokuwepo kwa wachezaji hao", amesema Dismas.
Pamoja na hayo, Dismas ameendelea kufafanua kwa kusema "Kelvin Yondani na Papy Kabamba hawa wote bado majeruhi mpaka hivi sasa, waliumia katika michezo iliyopita na kusababisha hata katika 'kariakoo derby' wasiweze kucheza kwa kiwango chao, Ajib mke wake ni mjamzito na anatarajia kujifungua muda wowote kutoka sasa hivyo inampasa abaki kumuangalia mke wake. Obrey Chirwa anaumwa ugonjwa wa malaria kwa hivyo jana alilazimika kuondolewa katika kikosi kutoka na kuumwa kwake".
Aidha, Kikosi cha Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, kimeshawasili mjini Algers nchini Algeria tayari kwa ajili ya kutupa karata yao ya kwanza hatua ya makundi kombe la shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao U.S.M Algers kesho jumapili Mei 06, 2018.
Kikosi kilichosafiri ya Yanga kina jumla ya wachezaji 17 akiwemo Youthe Rostand, Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Said Juma Makapu, Raphael Daud, Juma Mahadhi.
Wengine ni Emmanuel Martin, Yusufu Mhilu, Pius Buswita, Yohana Mkomola, Geofrey Mwashiuya, Abdallah Shaibu 'Ninja', Andrew Vicent, Juma Abdul, Haji Mwinyi na Pato Ngonyani.
No comments:
Post a Comment