DIAMOND KUWA MAKINI NA MITUNGI.. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday, 24 May 2018

DIAMOND KUWA MAKINI NA MITUNGI..

KWAKO staa namba moja wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, mambo yanakwendaje? Habari za mishemishe ya kila siku? Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima, ninamshukuru Mungu. Naendelea kupambana ndani ya nyumba, Global Publishers kuhakikisha kila siku gazeti lenye ubora wa hali ya juu linaingia mitaani.
Awali ya yote, nianze kwa kukupa pole na hongera kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Bila shaka utakuwa unafunga maana najua umelelewa katika misingi ya Dini ya Kiislam na mifungo mingi imepita nikikuona unafunga.
Baada ya salamu na pongezi hizo, moja kwa moja niende kwenye lengo la mimi kukuandikia barua hii. Kama mwanahabari nimekuwa nikipata malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya waandishi wenzangu kwamba siku hizi huenda ukawa umetopea kwenye matumizi ya pombe (mitungi).
Suala la pombe ni vigumu kulithibitisha hadi pale utakapopimwa kwa kifaa maalum, lakini kupitia matendo yako huenda yakaonesha dhahiri kwamba umelewa. Yawezekana mtu ukaamua kujichetua kama umelewa, lakini ukawa hujalewa, lakini kwa macho ya haraka, pombe huwa haidanganyi.
Juzikati, kwenye Ukumbi wa Life Club pale Mwenge jijini Dar palipokuwa na uzinduzi wa nyimbo za msanii wako, Mbosso, ulionekana kwenda nje ya mstari ulipovamia jukwaa.
Kuna wakati wenzako walionekana kutaka kukutoa jukwaani, lakini ukawa unagoma. Wapo waliodai kwamba walikuona ukipiga zile ‘chupa kubwa zile’ na ndiyo maana mambo yakawa yanaenda ndivyo sivyo. Diamond, lisemwalo lipo na kama halipo linakuja. Watu kusemasema hivi kuhusu pombe wamekuwa wakisema sana kuhusu wewe. 
Hakuna anayekukataza kunywa, lakini linapokuwa linakwenda kuharibu kazi yako hilo ndilo linakuwa tatizo. Hakuna asiyejua kwamba, linapokuja suala la pombe umakini wa kazi lazima upungue maana unaweza kufanya jambo ambalo hukulitarajia, lakini ukajikuta umeropoka.
Yawezekana hata zile tambo dhidi ya mpinzani wako ulizozitoa jukwaani pengine ungekuwa mzima, usingezitoa. Pombe haijawahi kumuacha mtu salama. Kama unakunywa, heshimu sana kazi. Kazi yako ni ya usiku hivyo ni vyema kuheshimu hilo.
Kwa umaarufu ulio nao, jina ulilonalo kama utaendekeza pombe ni rahisi sana kutumbukia shimoni. Niamini mimi, pombe ndiyo chanzo cha starehe nyingi kupindukia. Unaweza kujifunza kitu kupitia kwa Mr Nice aliyekuwa akizungukwa na warembo na kufanya anasa za kupindukia.
Nidhamu ya fedha huwa inapungua pindi tu unapokuwa mlevi kupindukia. Heshima yako inaweza pia kuondoka kwa sababu tu ya pombe.
Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na kufanyia kazi ushauri wangu.
Nikutakie mafanikio mema. Mimi ni nduguyo;

No comments:

Post a Comment