KWAHERI RAFIKI YANGU AGNESS.. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday, 24 April 2018

KWAHERI RAFIKI YANGU AGNESS..

Agness Gerald Waya
KWELI kila nafsi itaonja mauti. Bila kujali muonekano wa mtu, cheo chake, ustaa alionao au jinsi alivyokuwa akipendwa na watu, kila mtu atakufa. Ninaandika makala haya kwa uchungu nikikumbuka kifo cha rafiki yangu, Agness Waya Gerald almaarufu Masogange ambaye ninaweza kusema alikuwa ni mmoja wa mastaa asiyekuwa na shida au mawaa na mtu.

Nilikutana na Masogange miaka mingi kwa mara ya kwanza Sinza-Mori jijini Dar. Nakumbuka alikuwa na Janeth ambaye ndiye nilikuwa nikijuana naye kabla yake. Baada ya kutambulishwa, Masogange akaomba namba yangu ya simu na tangu hapo tulianza kuwasiliana mara kwa mara. Nilianza kumwandika habari mbalimbali kwenye magazeti yanayoongoza kwa kusomwa na wengi ndani na nje ya Bongo yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers.

Katika kujuana kwetu, Masogange aliamua kunishirikisha mambo kadha wa kadha ikiwemo uhusiano wake wa kimapenzi na kijana aliyeitwa Evance. Mara kwa mara alikuwa akiniita na kunishirikisha kuhusu mpenzi wake huyo kila wanapogombana na mwisho akaamua kunipa jina la ‘Dada Kitchen Party’. Hivyo akaniweka kuwa mmoja wa dada zake ambao anaweza kuwaeleza kila kitu.
Kuna wakati Masogange alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini mwaka 2013, akihusishwa na dawa zilizodaiwa kuwa za kuchanganyia madawa ya kulevya. Hatimaye aliwekwa mahabusu kwa miezi mitatu. Siku aliyoachiwa huru alinitumia SMS: “Dada yangu niko huru sasa, nakupenda.” Ujumbe huo ulinifanya niwe na furaha sana.

Masogange alikuwa si mwepesi wa hasira hata kidogo hata ukimkosea. Nakumbuka kuna habari niliandika ambayo mimi mwenyewe nilishuhudia kwa macho nyumbani kwake. Wakati huo alikuwa akiishi Sinza-Kwa Remmy. Habari hiyo ilikuwa na kichwa; ‘Masogange afanyiwa kitu mbaya na mwanaume’. Gazeti lilipotoka alinipigia simu asubuhi sana na kuniambia: “Dada Imelda sijapenda ulichofanya ila nimekusamehe.”

Katika hali ya kibinadamu, baada ya kupata ujumbe huo ndani ya moyo wangu niliumia sana. Lakini nilipompigia simu, sikuamini jinsi alivyoipokea kwa furaha kama kawaida yake na kwa sababu nilitaka kumuomba samahani, ilibidi niipotezee kabisa kwa sababu niliona hakuna sababu tena kwa kuwa tayari alishanisamehe kutoka moyoni. Aliniambia; ‘Ninatokea Posta na ninapita hapa ofisini kwenu (Global wakati huo tulikuwa Bamaga- Mwenge) kukuona’.

Tofauti na watu walivyomchukulia, Masogange alikuwa ni msichana mmoja mwenye aibu sana na kama hajazoeana na mtu, hawezi hata kumuangalia usoni akizungumza na hakupenda kabisa kujichanganya kwenye shughuli mbalimbali za wanawake wa mjini.

Kuna siku nilikuwa ninazungumza naye kuhusu mtoto wake, Samia na kumuuliza kwa nini hakupenda kumuweka kwenye mitandao ya kijamii kama wafanyavyo wasanii wengine au hapendi kujulikana kama ana mtoto? Akaniambia kuwa familia ya baba wa mtoto huyo haipendi kumuweka mtoto kwenye mitandao ya kijamii au vyombo vya habari. Alisisitiza’ ‘Dada Imelda naona hilo (la kutomuweka mtoto kwenye mitandao ya jamii) ni jambo zuri tu acha mimi nijulikane na kutukanwa, lakini siyo mwanangu’.

Miezi michache nyuma na baada ya kukumbwa na kesi ya kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya na mara kwa mara alikuwa akienda mahakamani kabla ya kuhukumu, nilikuwa nikiwasiliana naye kwenye simu na kumuuliza kuhusu mambo ya mahakamani na kuniambia alichokuwa akiomba tu kesi hiyo iishe ili aendelee na maisha mengine.

Katika hali ambayo haikuwa ya kawaida kati yangu na yeye, siku moja nilimpigia simu na kumuuliza habari za mahakamani, lakini hakuonekana mwenye furaha. Aliniambia; ‘Dada Imelda kama unataka kujua habari ya mahakamani ungewauliza waandishi waliokuwepo’. Baada ya hapo nilimtumia meseji nikam-wambia sivyo ninavyo-kuzoea.

Baada ya kum-tumia ujumbe huo naye alinijibu; ‘Dada yangu sitaki kuhojiwa’. Nikamwambia kwani mimi na wewe tukipigiana simu ni mahojiano tu? Ila hakunijibu tena ile meseji. Lakini ndani ya moyo wangu, Masogange ataendelea kuishi siku zote kwa sababu ni staa aliyekuwa na haiba ya kipekee kabisa…

No comments:

Post a Comment