DIAMOND ANAVYO ICHAKAZA DHAMANI YA ZARI NA HAMISA MOBETTO. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Saturday, 9 June 2018

DIAMOND ANAVYO ICHAKAZA DHAMANI YA ZARI NA HAMISA MOBETTO.

Watazame kwa umakini. Ni wazuri, zaidi ya uzuri wa haja. Sura zao zinapamba runinga na kurasa za mbele za magazeti. Ndivyo ilivyo kwenye kurasa za watu mitandaoni zanogeshwa na wao.

Wangeweza kuendesha vipindi vya runinga au mitindo na kuishi vyema. Wangeweza kucheza filamu yoyote ile na wakalipwa vyema. Na hata kudanga kimataifa wangetajirika.

Nyuso zao zina vipimo sahihi vya urembo. Macho yanaponya magonjwa yanayoletwa na mawazo. Vimo vyao vya kadiri havichoshi, zaidi ngozi zao huleta matumaini ya uhai.

Hata sauti zao zingesikika kwenye mwendokasi tusingepata mafuriko jangwani. Mvua zingeheshimu, lakini binadamu wenzao wameshindwa. Hawastahili kutukanwa lakini wanaoga matusi kila siku. Nitaeleza mbele.

Katikati ya kilio cha ukata mifukoni. Napokea simu ya mshikaji mmoja anataka nikaangalie uwekezaji wake huko Kimara. Sikutaka kupoteza muda wala kumuangusha nikamuibukia fasta.

Kajenga baa na ukumbi wa mikutano na harusi. Kuanzia hali ya hewa, mpaka harufu ya moshi kutoka jikoni ni pesa tupu. Jamaa kaweka pesa apate pesa. Nilipenda sana na kutamani kuwa na kitu kama kile.

Lakini furaha yangu ilitoweka kwa jambo alilomfanyia binti ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa jikoni. Ni aina ya manyanyaso wapatayo wahudumu wengi wa baa.

Alimuagiza chakula na vinywaji huku pia binti akiwa na ‘oda’ ya meza mbili za jirani, nilipotokea tu hapo hapo hata kabla hatujasalimiana bado akamtaka binti ageuze haraka ili asikilize upya.

Binti huku akielekea kaunta akaomba akamilishe ‘oda’ moja ndipo atusikilize upya. Likawa kosa kubwa na jamaa kuanza kufoka kama fuko kwa madai ya kudharauliwa. Wote tuliduwaa.

Inaonesha binti hakufahamu bado kuwa yule ni nani pale. Ujivuni wa pesa na kutaka sifa kwa wageni, akamuita mpishi jikoni ambaye ni muajiri wa binti, akaagiza amueleze binti kuwa yeye ni nani pale.

Jamaa akafanya kama alivyoagizwa haraka sana akamfuata binti pale kaunta. Ajabu neno tulilolisikia vyema wageni wote kutoka kwa binti ni: “Hata kama ndiyo mwenye mali asinitishe, kwani mimi mtumwa?”

Kilichofuata jamaa akauliza anachodai yule binti, kisha akatoa keshi na kumlipa huku akiamuru atoe pua yake pale milele amina. Binti akapokea akasunda kifuani na kuondoka kijeuri naye.

Iliniuma sana na sikusubiri kushuhudia zaidi. Wakati akigeuka kuongea na wengine nikazuga kama naenda msalani kisha nikatokomea jumla. Sipendi mazoea na wapuuzi.

Hizi ni tabia za wamiliki wa baa wengi wale malofa wa akili. Mhudumu wa kike hugeuzwa chombo na siyo binadamu mwenye haki za kiutu. Hudharauliwa na kuwalazimisha wawe sehemu ya kiburudisho cha wateja.

Wahudumu wa kiume hawavalishwi sare za kuonesha six packs, kama kiburudisho kwa wateja wa kike. Lakini wa kike wanapewa sare za nusu utupu mapaja nje kuburudisha wateja wa kiume.

Na hii siyo kwa wamiliki wa baa pekee. Ni jamii nzima hasa kwa nchi hizi masikini, bado tupo gizani kwa kufubaisha akili zetu ziendelee kuamini kuwa mtoto wa kike ni bidhaa au chombo.

Wanawake wanaojiuza wanapewa majina yote mabaya, wanunuzi ambao ni wanaume hawaguswi. Utadhani wanawake miili yao wanaziuzia mbuzi za albadiri zilizotapakaa kule mitaa ya Kinondoni.

Na ndiyo maana thamani ya bikira ni kwa ajili ya mwanamke tu, hakuna mwanaume atakaye ulizwa kama ni bikira. Kwa akili zetu mtoto wa kiume ni halali kutenda uzinifu kabla ya umri wa utu uzima.

Malezi mabovu kwa watoto lawama zote ni kwa ‘single mothers’, lakini ‘single fathers’ hawapewi lawama. Wanaonekana hodari vidume wa kutembeza bakora kila mtaa.

Binti akipata mimba baba anakasirika sana, akiwa na boyfriend tu anakasirika mno. Lakini kijana wake wa kiume akiwa na girl friend hakasiriki. Walioendelea mbele zaidi wanatoa na pesa za guest.

Ndoa ikivunjika lawama kwa mwanamke, ataitwa ameachika hata kama yeye ndo amemuacha mumewe. Tumeamua kumfanya kiumbe wa kike awe dampo la kutupia lawama zote.

Dada akiona mdogo wake wa kiume ana girl friend hakasiriki, ila mdogo wa kiume akiona dada ana boyfriend anakasirika. Na wengine hutafuta ‘masela’ wake wanamvizia wampige boy friend wa dada yake.

Mwanaume anamtuma mdogo wake wa kike akamuunganishie kwa rafiki yake, lakini ni ngumu kaka kumuunganishia mdogo wake wa kike kwa masela. Hiyo vita yake ni kubwa.

Mwanaume akifanya mapenzi anaonekana rijali, ila mwanamke akifanya mapenzi anaonekana malaya. Na hii hata kwa wanawake wenyewe wanaona mwenzao hafai ila mwanaume sawa sawa tu.

Hilo jambo sijajua bado kama ni asili ama kitu gani. Kama huamini kafanye mapenzi na mdogo wa kike wa rafiki yako, urafiki unaweza kutoweka kama nyimbo za Mr Nice.

Lakini haya ni kwetu Afrika, Wazungu binti wa miaka 16 wazazi wanaruhusu awe na boyfriend siyo kwa ngono lakini, mpaka akifikisha miaka 18 ndiyo ruksa.

Kwetu hata mwanamke ambaye kishazalishwa, bado kaka mtu au baba kama siyo mjomba huumia kuona yuko na kidume. Yaani akionekana naye upenuni atasakiziwa hata mbwa au kuitiwa mwizi.

Kuna jamaa aliwahi kuniambia kuwa

Wazungu wamekumbwa na laana ya mapenzi ya jinsia moja, kwa hiyo ikitokea mwanaye akawa na uhusiano na jinsia tofauti kwao ni kheri sana.

Lakini nilipojaribu mwenyewe kufuatilia sana nikagundua kuwa, wenzetu wanawaza vitu vikubwa haya mambo ya nani anatoka na nani walishavuka daraja hilo karne nyingi nyuma.

Hamisa Mobetto na Zarina Hassan ‘Zari’. Warembo wenye urembo wao ambao wote wameamua matumbo yao kumbebea mimba msela mmoja wa Tandale. Umefuatilia sakata lao?

Zari anatukanwa mitusi mitandaoni na mashabiki wa Hamisa. Na vile vile Hamisa naye anakoga mitusi ya kutosha kutoka kwa mashabiki wa Zari. Yaani imekuwa kama mchezo wa kitoto wenye utoto ndani yake.

Mama Diamond na dada zake nao wanavimbiwa mitusi kabla hata ya kufuturu. Ndivyo ilivyo kwa mama yake Hamisa naye anayaoga matusi mengi tu. Inasikitisha.

Umegundua kitu hapo? Hamisa anatukanwa na wapuuzi eti kuingilia penzi la mwenzake. Zari naye anatukanwa kwa sababu wanazozijua wenyewe majuha wa mitandaoni. Watu wameamua kuondoa stress zao kwa hawa wanawake.

Kidume chenyewe kimetulia. Hakiguswi. Yaani utadhani Hamisa na Zari wamezaa na mtoto mdogo au mwendawazimu ambaye hajui kitu hivyo hana makosa na hatakiwi kulaumiwa.

Wanashambuliwa wazazi wa kike wa pande zote mbili. Lakini Diamond kama hayupo vile hapa duniani. Na wanaowatukana wanawake hawa asilimia tisini ni wanawake wenyewe. Matusi yenyewe mengi ni ya viungo vya kina mama.

Kwa namna hii na akili hizi, mfumo dume kwa sisi Waswahili wa dunia ya tatu huku, hautaisha milele amina mpaka shetani atakapoonekana mitaa ya posta akinywa dafu au baa akiagiza bia na nyama choma.

No comments:

Post a Comment