Wakazi wa Kata ya Moita wameombwa kumchagua mgombea wa CCM ili wapate maendeleo na kuachana na ahadi alizowapa, Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati kuu, Chadema, Edward Lowassa.
Lowassa aliyewahi kuwa mbunge wa Monduli ndiye aliyezindua kampeni za udiwani za Chadema katika kata hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwaahidi wananchi kuwa hatawasahau na ataendelea kushirikiana nao, kwani aliwaacha wakiwa tayari wana umeme, maji na shule mbili za kata.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe akizungumza katika kampeni eneo la Moita Bwawani, alisema wananchi wasidanganyike.
Mdoe alisema kwamba wakimchagua mgombea wa CCM, Prosper Meyani kero zao zitapatiwa ufumbuzi, ikiwamo kero ya maji na barabara.
“Msidanganywe na Chadema, hawawezi kutatua kero zenu, alikuwepo diwani wao, hadi amejiuzulu, mbunge wa zamani Lowassa hivi sasa hawezi tena kuwasaidia,” alisema.
Awali, aliyekuwa diwani wa kata hiyo na kujiuzulu, Edward Sapunyo alisema aliamua kujiuzulu baada ya kunyimwa ushirikiano na madiwani wa Chadema.
Alisema kila mradi ambao alikuwa anaomba katika kata hiyo alinyimwa na hivyo akaona hana sababu ya kubaki bali arejee CCM.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Sapunyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli kupitia CCM, alisema chaguo sahihi katika kata hiyo ni mgombea wa CCM.
Halmashauri ya Monduli hadi sasa inaongozwa na Chadema kutokana na kuwa na madiwani 18 na CCM madiwani tisa.
No comments:
Post a Comment