Niyonzima,Mavugo wapigwa chini - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Monday, 1 January 2018

Niyonzima,Mavugo wapigwa chini

MASHABIKI wa Simba huenda wakashtuka kusikia taarifa hii, lakini ukweli ni kwamba benchi la ufundi la klabu hiyo limeamua kuwatema kikosini nyota wawili; Laudit Mavugo na Haruna Niyonzima kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi.

Simba ambayo jioni ya leo Jumanne inatarajia kutupa karata yake katika michuano hiyo kwa kuvaana Mwenge, iliwatema wachezaji hao katika msafara wa wachezaji 24, huku ikiwajumuisha Emmanuel Okwi na beki Shomary Kapombe waliokuwa majeruhi.

Kapombe hajaichezea Simba hata mechi moja tangu ilipomsajili kutoka Azam mapema msimu huu, lakini amerejea na ataanza mazoezi na wenzake kwa ajili ya michuano hiyo ambayo Simba imepania kubeba taji.
Kocha wa Simba, Masudi Djuma, amesema Mavugo na Niyozima wameachwa kwa vile wana matatizo. Mavugo bado yupo kwao Burundi na Niyonzima anauguza maumivu ya kifundo cha mguu.

Djuma alisema Mavugo alienda Burundi baada ya kumalizika kwa Kombe la Chalenji na amemshauri aje kipindi cha maandalizi ya Ligi Kuu Bara, ikiwa na maana ataikosa michuano ya Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
“Simba imesajili wachezaji wengi na kukosekana kwa Mavugo na Niyonzima sio shida, kuna wengine ambao watacheza katika nafasi zao na kazi ikafanyika kama ilivyokuwa kwenye mechi ya ligi dhidi ya Ndanda,” alisema.

“Muda wa kujiandaa kwenye mashindano haya ni mdogo kutokana tumecheza mechi ya ligi mkoani, hatujapumzika tunakuja huku hatuna muda hata wa kufanya mazoezi tunatakiwa kucheza mechi, hivyo tutapambana kadiri ya mazingira.”
Kocha Djuma alisema licha ya ratiba kuwabana lakini wamedhamiria kufanya vizuri kwenye michuano hii ili kurejesha taji walilopokwa na Azam msimu uliopita.

NIYONZIMA ANENA
Niyonzima amesema maumivu ya kifundo cha mguu ndiyo yamemsumbua asisafiri na timu.
“Nitabaki hapa Dar ili kupata matibabu zaidi na Mungu akijalia nitakuwa na timu wakati wa kujianda na mechi yetu ya Ligi Kuu dhidi ya Singida United,” alisema Niyonzima.

KAPOMBE NDANI
Wakati Mavugo na Niyonzima wakishindwa kujumuishwa katika kikosi hiko cha Simba kwa sababu zao, beki wa kulia Shomary Kapombe, yupo katika kikosi hicho na ataanza mazoezi kwa mara ya kwanza na wenzake visiwani humo.

Djuma alisema amefurahishwa na ujio wa Kapombe, japo hajamuona hata siku moja, lakini ana imani kuwa ameshakuwa fiti na atafanya naye mazoezi na kama atakuwa fiti zaidi atampa nafasi ya kucheza.

Simba imetua Zanzibar na wachezaji 24 na leo jioni inashuka uwanjani kucheza na Mwenge kabla ya Yanga kuivaa Mlandege saa 2:15 usiku. Mechi zote zitapigwa Uwanja wa Amaan.

No comments:

Post a Comment