MABOSI na mashabiki wa Yanga mpaka sasa bado hawaamini kama timu yao imepigwa tena kwa mara ya tatu na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Lakini ukweli ni kwamba juzi Jumapili walichezea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa vijana hao wa kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije, huku straika chipukizi, Habib Haji Kiyombo akiendelea kuwatia maumivu Jangwani kwani ndiye aliyefunga yote.
Mwanaspoti lilikuwapo uwanjani hapo likiushuhudia mchezo huo mwanzo mwisho na linakuletea dondoo chache ya kilichojiri uwanjani na jinsi ilivyokuwa lazima Yanga inyukwe katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara.
Kivipi?
REKODI DAKIKA 270
Kama hujui ni kwamba Yanga imeweka rekodi jijini Mwanza kwa kufikisha dakika 270 kwenye mechi zake dhidi ya Mbao za Kirumba bila kufunga bao lolote, achilia mbali kupata ushindi. Hii ni tofauti na ilivyozoeleka enzi zile ikiifuata Toto Africans ama timu nyingine.
Msimu uliopita Yanga ilichezea bao 1-0 katika pambano la Kombe la FA na ikapigwa tena kwa idadi hiyo ya bao kwenye ligi kabla ya juzi Kiyombo kuwaumiza kwa mabao mawili. Yanga imefungwa kwa sababu ya presha yake.
Tangu Mbao ipande Ligi Kuu haijawahi kufungwa na Yanga Kirumba, hivyo wageni wao waliingia wakiwa na kiu ya kisasi, wakaumia.
NGUMI NJE NJE
Kuthibitisha Yanga hawakutarajia kipigo, mara baada ya mchezo makomandoo wake walianza kulaumiana kabla ya kuamua kuzichapa.
Walizichapa kavukavu kabla ya polisi kuingilia na kuwafurusha uwanjani hapo, huku ikisemekana kuna mambo waliyakosea kupitia mipango yao ya nje ya uwanja hasa mambo ya kishirikina na ndio maana wakaamua kulianzisha.
Hata kabla ya mchezo, makomandoo hao walionekana kuwa wababe, lakini wakasahau kuwa soka huwa linachezwa uwanjani na soka sio ngumi.
KIYOMBO ANAJUA BWANA
Kiyombo alionyesha kuwa yeye ndiye anayeijulia Yanga. Msimu uliopita aliwatungua hapo hapo Kirumba na kabla ya mchezo wa juzi alitamba lazima awaumize tena. Ikawa kweli.
Dakika 45 za kwanza mabeki wa Yanga Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wakishirikiana na wale wa pembeni kina Gadiel Michael na Juma Abdul kabla ya Hassan Kessy, walijitahidi kumzuia Kiyombo na wenzake.
Hata hivyo anayejua anajua tu, kwani Kiyombo alitumia makosa ya mabeki hao kwa muda wa robo saa tu kuwatia adabu kwa kufunga mara mbili kwa juhudi zake na kumfanya chipukizi huyo kumkaribia Emmanuel Okwi kwa mabao.
Kiyombo aliyefunga mabao matano pekee yake katika mechi ya Kombe la FA wiki iliyopita, amefikisha mabao saba ya Ligi Kuu, Okwi wa Simba anayo manane.
AJIB, CHIRWA NI PENGO
Kila aliyekuwa uwanjani alilishuhudia pengo la dhahiri la nyota watano wa Yanga, hasa kwenye safu ya ushambuliaji. Pengo la Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa lilionekana wazi kuliko la Thabani Kamusoko, Donald Ngoma na mabeki visiki, Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Katika mchezo mgumu kama huo wa juzi, Yanga ingewezaje kutoka salama hata kama ilikuwa na Amissi Tambwe aliyerejea kutoka benchi la majeruhi. Papy Kabamba Tshishimbi alikosa mtu wa kusaidiana naye kuiadhibu Mbao.
Tambwe alishindwa kabisa kuonyesha kiwango chake baada ya kuthibitiwa na mabeki wa Mbao waliokuwa wakiongozwa na nahodha wao, Yusuph Ndikumana, ambaye ni raia mwenzake kutokea Burundi.
SIMBA ILIONGEZA PRESHA KIRUMBA
Upinzani wa Simba na Yanga upo popote nchi nzima. Mashabiki wa Simba wa jijini hapa walijazana kwa wingi kwenye jukwaa la Mbao wakiwa na jezi zao nyekundu na kuwajaza upepo wachezaji wa timu hiyo yenye maskani yake wilayani Ilemela.
Muda wote wa mchezo huo mashabiki hao wa Simba walikuwa wakiimba na kuishangilia Mbao na hata mchezo ulipomalizika walikuwa na furaha tele, ila bahati mbaya ni kwamba walichezea kichapo kutoka kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa na hasira.
Wachezaji wa Yanga walijikuta wakicheza kwa presha kubwa ndani na nje ya uwanja na matokeo yake wakatoka uwanjani kinyonge wakipoteza mchezo huo.
NINJA AZUA UTATA
Kama kuna mchezaji aliyekuwa gumzo katika pambano hilo baada ya Tshishimbi na Tambwe basi ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
Achana na aina yake ya uchezaji na hata kukimbia, Ninja aliwachanganya mashabiki waliokuwapo Kirumba akifananishwa na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Mashabiki hao walikuwa wakibishana kuwa Ninja ndiye Cannavaro, lakini baadaye walikuja kubaini kuwa wamemfananisha tu, ila ni watu wawili tofauti. Lakini kwa hakika Ninja na Cannavaro wanafanana sana hata uchezaji.
Hata hivyo beki huyo alishindwa kuvaa viatu vya Cannavaro ama Yondani na haikuwa ajabu alishindwa kumzuia Kiyombo asifunge akiwa sambamba na Dante.
MBAO WALIKUWA VIZURI
Katika dakika 90 za pambano hilo, Mbao FC walionekana kuwa vizuri zaidi kuliko Yanga, hata kama wapinzani wao walikuwa na wachezaji wengi wazoefu.
Wachezaji wa Mbao hasa James Msuva, Amos Charles na Emmanuel Mvuyekule wasingekuwa na papara katika kipindi cha kwanza na hata cha pili, wangewapiga nyingi Yanga.
Walisumbua mno wakishirikiana na Kiyombo na hata alipoingia Boniface Maganga walizidi kuongeza kasi kwa Mbao dhidi ya Yanga na ndio maana haikushangaza mabao mawili kutinga mbavuni mwa kipa Youthe Rostand.
Rostand na uimara wake katika mechi zote alizoidakia Yanga, juzi alithibitisha kuwa ni mbovu kwa mipira ya chini aliyofungwa na Kiyombo.
Ukiondoka mapengo ya nyota waliokosekana Yanga, udhaifu wa safu ya ulinzi na hata kutokuwepo kwa Kocha Mkuu, George Lwandamina, ukweli unabaki kuwa Mbao walikuwa vizuri zaidi ya Yanga na ndio maana ni dhahiri ilikuwa lazima Wana Jangwani wakalishwe. Mbao inastahili ushindi huu.
No comments:
Post a Comment