Kwa Kichuya hakuna Okwi wala Ajibu - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday 9 November 2017

Kwa Kichuya hakuna Okwi wala Ajibu

WINGA wa Simba, Shiza Kichuya, si mtu wa mzaha kwani ameweka rekodi ya maana Ligi Kuu Bara ambayo imewashinda mastaa wenzake; Emmanuel Okwi na Ibrahim Ajibu.

Kichuya alifunga bao pekee la ushindi dhidi ya Mbeya City Jumapili iliyopita na kufikisha mabao matano msimu huu, ambayo yamemfanya kuwa na rekodi ya kipekee.

Ndio, Okwi ndiye kinara akiwa na mabao manane na Ajibu ameshatupia matano mpaka sasa akiwa na Yanga, lakini wote wanasubiri kwa winga huyo.

Kwanza, Kichuya amewafunika Okwi na Ajibu kwa kuwa mshambuliaji pekee aliyefunga katika mechi nyingi zaidi msimu huu. Amefunga katika mechi tano wakati Okwi na Ajibu wamefunga katika mechi nne.

Kichuya amefunga mabao yake hayo dhidi ya Ruvu Shooting, Mbao FC, Stand United, Yanga na Mbeya City.

Winga huyo machachari zaidi nchini, ameweka rekodi pia ya kufunga katika mechi tatu mfululizo dhidi ya Mbeya City. 

Aliwafunga kwenye mechi zote mbili za msimu uliopita kabla ya kuwafunga tena juzi Jumapili.

Kichuya amemfunika Okwi pia kwa kuwa mchezaji wa Simba aliyefunga mabao mengi zaidi ugenini, akiwa amefunga mara tatu msimu huu wakati staa mwenzake huyo hajafunga ugenini hata mara moja.

Kutokana na kasi yake hiyo, nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema Kichuya amekuwa mchezaji wa kujiongeza hasa katika kufunga, jambo ambalo linamfanya kuwa juu ya wachezaji wote wanaocheza katika nafasi kama yake.

“Ana nidhamu na anaifanya kazi yake kwa ufasaha. Bado hajarudi kwenye makali yake ya msimu uliopita lakini ni hatari, anafunga licha ya kwamba anacheza pembeni,” alisema Mgosi aliyeshinda mataji manane na Simba.

“Ni mchezaji ambaye anajituma muda wote, yeye pamoja na Mzamiru Yassin wana kitu cha ziada, siku zote huwa nasema watafika mbali.

“Kama wachezaji wote kikosini humo wangekuwa wanacheza kama wao, Simba isingeshikika.”

No comments:

Post a Comment