MWIGULU:SERIKALI HAIJUI KUWA BEN SAANANE YUPO HAI AU AMEKUFA. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday, 28 September 2017

MWIGULU:SERIKALI HAIJUI KUWA BEN SAANANE YUPO HAI AU AMEKUFA.

Mwigulu Nchemba.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema Serikali haijui kama Ben Saanane alikufa au yuko hai, lakini Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta ili kujua kilichotokea. Saanane ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema na Msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alitoweka tangu Novemba 2016.

Amesema hayo leo Alhamisi katika kipindi cha
Clouds 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds alipojibu swali aliloulizwa na mtangazaji wa kipindi hicho iwapo Ben Saanane yuko hai au amefariki dunia.

“Ni ngumu kusema kama Ben Saanane yuko hai au amefariki kwa sababu bado hatujui nini kilimpata,” amesema .

Amesema Polisi wanaendelea kumtafuta kwa kuwa ni mtu aliyepotea. Amewataka watu wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwake watoe ushirikiano.

“Msidhani kwamba Serikali haifanyi chochote, suala ambalo linahusisha maisha ya mtu hatulipuuzi tunaendelea na upelelezi,” amesema. Kuhusu mtu aliyemtishia bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema wamejiridhisha kwamba hakuwa polisi.

“Kwanza tulitaka kufahamu yule jamaa aliyefanya kitendo kile kama alikuwa polisi lakini tulikuja kufahamu kwamba hakuwa polisi,” amesema.

Amesema katika mazingira kama yaliyotokea yanaweza kutumiwa na mhalifu yeyote kufanya alichokifanya. Amesema bado wanalifanyia uchunguzi suala hilo. Hata hivyo, Mwigulu hakujibu swali aliloulizwa iwapo mtu huyo amekamatwa au hajakamatwa hadi sasa.

Machi 23, Nape alitishiwa kwa bastola wakati alipofika katika Hoteli ya Protea kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari. Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya  Rais John Magufuli kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyomwondoa Nape kwenye nafasi ya uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

No comments:

Post a Comment