Mshambuliaji mpya wa Simba, Nicholaus Gyan amefunguka kuwa anajua benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha wake, Joseph Omog linahitaji mabao mengi kwenye msimu huu wa ligi kupitia kwake,
hivyo yeye ameshajiandaa kulibeba jukumu hilo kwa kufunga kila atakapopata nafasi ya kufanya hivyo.
Mghana huyo ambaye anaungana na raia mwenzake, James Kotei, amesajiliwa kwenye kipindi hiki kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya Simba, baada ya mabosi wa timu hiyo kuridhishwa na kiwango chake alichokionyesha akiwa na moja ya klabu za kwao.
Gyan ameshaitumikia Simba michezo miwili ya kirafiki mmoja wa Simba Day dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda na Hard Rock ya Pemba ambapo kwenye michezo hiyo tayari ameshafunga bao moja.
Akizungumza straika huyo alisema: “Najua watu wa hapa kuanzia viongozi hadi makocha wameweka imani kwangu kwamba nitawafungia mabao kama nilivyokuwa nafanya nyumbani na sababu hiyo ndiyo maana walinisajili na kunileta kuungana na wao msimu huu.
“Kwangu naamini sitashindwa kufanya hivyo kwa sababu nilijipanga zamani kuhakikisha nalifanya hilo na pia ukiangalia suala la kufunga kwangu halijawahi kuwa tatizo, tangu natoka nyumbani nimekuwa nafunga na hata hapa nilipo nitaendeleza makali ya kufunga,” alisema Mghana huyo.
Aidha, Gyan amesema kuwa amelipata begi lake lililokuwa na vifaa vyake vya michezo ambalo lilipotea uwanja wa ndege alipowasili Dar es Salaam wikiendi iliyopita.
No comments:
Post a Comment