MAKOCHA Joseph Omog wa Simba na Hans Van Pluijm wa Singida United ni miongoni mwa mabosi wanne wa timu za Ligi Kuu ambao wameishika ajira ya kocha wa Yanga, George Lwandamina.
Yanga ambayo ipo nafasi ya sita Ligi Kuu itacheza mechi zake nne zijazo dhidi ya Kagera Sugar inayofundishwa na Mecky Maxime, Stand United ya Niyongabo Abbas, Simba ya Omog na Singida ya Pluijm.
Mtihani mgumu kwa Lwandamina ni kwamba mechi tatu kati ya hizo atacheza ugenini ikiwemo kuzindua Uwanja wa Namfua wa Singida United ambao Pluijm ameapa kwamba hakuna mtu wa kuwafunga pale kwao.
Rekodi zinaonyesha kuwa hali ni ngumu zaidi kwenye mchezo dhidi ya Simba kwani tangu Omog alipokabidhiwa timu hiyo mwaka jana hajapoteza mchezo wowote dhidi ya Yanga katika mechi nne walizokutana ambapo ameshinda moja na sare tatu.
Yanga ipo Kaitaba leo Jumamosi kuikabili Kagera ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 6-2 mwaka jana lakini kwa Stand ilikumbana na kipigo cha bao 1-0.
Changamoto kubwa inayowakabili mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ni upachikaji wa mabao ambapo msimu huu wamefunga mabao manne tu katika mechi tano za awali, tofauti na msimu uliopita ambapo katika mechi tano za awali walifunga mabao manane.
Kocha msomi zaidi nchini, Professa Mshindo Msolla amesema; “Ni ratiba ngumu sana kwa Yanga. Kwa namna timu yao inavyocheza sasa ni ngumu kusema itakwenda kupata matokeo mazuri katika michezo hiyo, pengine baada ya mechi hizi kunaweza kuwa na mgogoro mkubwa katika timu hiyo.
“Ni kweli kwamba kocha Lwandamina ana matarajio makubwa na kurejea kwa Amissi Tambwe lakini sitarajii kuona akifanya makubwa kwenye hii michezo.
Ndiyo kwanza ametoka majeruhi, atafanya vizuri baadaye,” alisema Msola aliyewahi kuinoa Stars.
Kocha wa zamani wa Mbeya City, Kimondo na Panone, Maka Mwalwisi alisema; “Yanga bado iko kwenye mabadiliko makubwa ya kiuchezaji. Lwandamina anajaribu kubadili mfumo waliokuwa nao Yanga wakati wa Pluijm na kuleta mfumo mpya, lakini bado hali yao siyo nzuri. Kama watu wa Yanga watakosa uvumilivu inaweza kumgharimu.”
“Lwandamina ni kocha mzuri lakini naamini Yanga walifanya kosa kubwa kumwondoa Pluijm. Hili ndilo linawapa wakati mgumu sasa. Inabidi wawe na subira atengeneze timu anayoitazamia,” alisema Mwalwisi.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina amesisitiza kwamba bado ni mapema kufanya kazi kwa presha lakini ameandaa mkakati maalumu wa kupambana na mechi za ugenini ambazo ndiyo zinazowakwaza.
No comments:
Post a Comment