SHETANI ALIYE MPITIA BUSWITA KUSAINI MARA YA PILI,AFE KWA TULIPO FIKIA. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday 7 September 2017

SHETANI ALIYE MPITIA BUSWITA KUSAINI MARA YA PILI,AFE KWA TULIPO FIKIA.

TAYARI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeeleza kuwa kiungo mpya wa Yanga, Pius Buswita anaweza kuanza kuitumikia timu hiyo mara moja baada ya suala lake kumalizwa kwa malipo.
Yanga wanatakiwa kurudisha kitita cha Sh milioni 10 ambazo Buswita alichukua akiwa Mbao FC lakini baadaye akachukua fedha tena na kusaini Yanga na mwisho amesababisha mtafaruku ambao ulipelekea yeye kusimamishwa kucheza msimu mzima.
Kwanza nianze kuwapongeza TFF kufikia hadi kulimaliza suala hilo kwa kuwa Buswita anaweza kucheza tena na vizuri kwake, familia yake, mashabiki na hata sisi wadau wa soka kwa kuwa ni kijana ambaye ninaamini akijituma, baadaye atakuwa msaada kwa taifa letu.
Kumuacha Buswita asicheze haikuwa kumkomoa, badala yake kumtia adabu ili wenye tamaa au tabia ya kutokuwa makini kama yeye wasijitokeze tena.
Nilishawahi kuandika kuhusiana naye na nikaeleza wazi kwamba hakuwa sahihi kama ambavyo upande wake ulikiri kwamba shetani alimpitia hadi kufanya kitendo cha kupokea fedha kutoka kila upande huku akijua kisheria lilikuwa kosa.
Katika makala hiyo niliwasisitiza Simba kumsaidia kama wangeona inafaa na yeye angeonyesha uungwana kwamba alikuwa tayari kurejesha fedha na alikuwa akijutia kitendo alichokifanya.
Lakini nikaweka msisitizo bila ya woga kwamba, kama ataonyesha hajali, basi aachwe atumikie adhabu. Siku chache baadaye, nilielezwa kulikuwa na mazungumzo ambayo yalihusisha ubinadamu lengo likiwa kulimaliza suala hilo kirafiki kwa lengo la kumsaidia Buswita.
Hapo tuwapongeze Simba waliokubali kukaa katika jambo hilo ambalo hata wangegoma kwa upande wa haki walikuwa nayo na ingekuwa ni sahihi tu kufanya namna hiyo.
Lakini wameonyesha wamepevuka zaidi kisoka ukiachana na watu wachache waliokuwa wametanguliza ushabiki wa kupindukia na kutaka kuonyesha kama vile Buswita hakuwa na kosa hata kidogo na badala yake Simba ndiyo wanaotaka kumbania, jambo ambalo lilikuwa ni kumfanya mchezaji huyo azidi kushindwa kujielewa kabisa akiamini anaonewa wakati shetani wake ndiye aliyesababisha hayo yote yaliyotokea.
Sote tunajua namna watu makini wanavyoweza kuepuka mambo mengi ambayo baadaye yanaweza kuwa tatizo hapo baadaye. Hivyo badala ya kulikuza tatizo zaidi kwa kuonyesha wachezaji wameonewa au kuingiza ushabiki ni vizuri kuambiana ukweli.
Hili la Buswita limekwisha sasa na kama ni mtu aliyekuwa amekosea kweli atakuwa amejifunza. Hivyo itakuwa poa zaidi wasitokee wengine kufanya makosa kama hayo na kukosea halafu mwisho wamsingizie shetani kwamba alikuwa sababu kuu ya wao kukosea.
Wakati tunawakanya wachezaji, hata upande wa viongozi nao wanapaswa kubadilika na kuachana na mambo ya kizamani kufanya usajili wa kishabiki au kutaka kuzidiana kete kwa kukomoana.
Kama klabu inamtaka mchezaji na wengine wamemuwahi, kuna kila sababu ya kuangalia taratibu sahihi za kufanya. Kama zitashindikana basi inaweza ikaangalia njia mbadala kwa kuwa wachezaji wako wengi sana.
Mchezaji kuwa amesajiliwa na timu moja, halafu nyingine inakwenda kumsajili kwa kuwa inajiamini iko vizuri kwa fitina ni mambo yaliyopitwa na wakati kwa kuwa kujivunia fitina kipindi hiki ni kuonyesha umechelewa kwa kiasi gani.
Nafasi ya kulizika suala la mchezaji kuwa amesaini timu mbili iwe sasa. Buswita awe wa mwisho na ikiwezekana muda huu tunaopoteza kujadili haya mambo tuutumie kujadili mambo mengine ya maendeleo ambayo huenda yatawasaidia zaidi wachezaji wenye na mpira wa Tanzania.
Viongozi kuna mambo mengi sana ya msingi yanayoweza kuzaa mafanikio ambayo hamjawahi kuyafanya. Hivyo vizuri muanze sasa na kuachana na ujinga huu wa kugombea wachezaji kwa makusudi.
NA ERICK PICSON.

No comments:

Post a Comment