KUFUATIA tukio la utekaji watoto Arusha , imeelezwa kuwa Askari wa Jeshi la Polisi hawakufika eneo ambalo watu wanaodhaniwa kuwa ni watekaji walifika kujaribu kukutana na mmoja wa wazazi wa watoto waliotekwa na ambao baadaye alikutwa ndani ya shimo la majitaka wakiwa wamekufa.
Watoto hao, Moureen Daudi , mwenye umri wa miaka sita na Ikram Salim (3) , walitekwa wiki iliyopita. Watoto wanne walitekwa katika matukio tofauti, lakini wawili waliachiwa.
Mmoja wa watekani alikamatwa mwishoni mwa wiki akiwa Geita na kusafirishwa hadi Arusha kwa ajili ya hatua za kisheria.
Kassim Salum , ambaye ni mzazi wa Ikram alisema kabla ya mtoto wake kuuawa alipigiwa simu usiku na watu waliomtaka wakutane katika uwanja wa wazi uliopo Olasiti ili awape fedha walizotaka ikiwa ni sharti la kumuachia mtoto wake.
Mzazi huyo alieleza kwamba baada ya kufika katika uwanja huo ulio jirani na Shule ya Msingi ya Lucky Vincent , aliwaona vijana zaidi ya watano.
Alisema baada ya kuwaona alifanya juhudi za kuwajulisha polisi ili wafike eneo hilo, lakini hawakufika.
“Licha ya kujitahidi kuwatafuta polisi, hawakufika,” alisema Salum.
“Nililazimika kuondoka eneo hilo kutokana na kuhofia usalama wangu.”
Tayari, jeshi hilo linamshikilia Samson Petro (18) ambaye alikamatwa Septemba 2 mkoani Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Arusha, Charles Mkumbo alisema baada kuibuka kwa matukio ya utekaji, jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi walianza juhudi za pamoja zilizofanikisha kukamatwa kwa kijana huyo.
Mkumbo alisema kwamba katika mahojiano, kijana huyo alikiri kuwateka watoto hao na kisha kuwaua kwa kuwatumbukiza katika shimo la majitaka lililopo katika nyumba iliyoko Mtaa wa Olkeryan ambayo ujenzi wake haujakamilika.
Alisema baadaye walimchukua kijana huyo kwenda eneo la tukio na kukuta miili ya watoto hao ikiwa inaelea.
Kamanda Mkumbo alisema mbali na matukio hayo mawili, mnamo Agosti 28 saa 11:45 asubuhi katika maeneo ya Kwamromboo, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwateka watoto wengine wawili; Ayubu Fred (3) na Bakari Seleman (3) ambao baadaye aliwaachia.
Kamanda Mkumbo alisema jeshi hilo pia linamshikilia wakala wa fedha wa kampuni moja ya simu ambaye alitoa Sh300,000 kwa mtuhumiwa.
Kuhusu mazishi ya wawili hao, mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Olkerian, Daudi Safari alisema taarifa kamili zitajulikana baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika
No comments:
Post a Comment