MSEMAJI wa Klabu ya Simba, Haji Sunday Manara amefunguka kwa kina kuhusu tetesi zinazosambaa mitandaoni kwenye vyombo vya habari kuwa klabu hiyo inataka kuachana na kocha wake mkuu, Joseph Omog kwa kile kinachodaiwa kuwa ana kikosi kikubwa na cha gharama kubwa lakini amekuwa akipata matokeo yasiyoridhisha kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania iliyoanza mwezi uliopita.
Akifungukia tetesi hizo jijini Mwanza leo, wakati timu hiyo ikijiandaa na mchezo dhidi ya Stand United ya mjini Shinyanga utakaopigwa weekend hii, Manara amewatoa hofu mashabiki wa Simba akiwaeleza kuwa Kocha huyo ni mzuri na ana mifumo itakayowasaidia kuibuka mabingwa kwenye michuano inayoendelea.
“Hatuiwezi kuachana na kocha Omog, naomba hilo mliondoe kabisa akilini mwenu, suala la matokeo linategemeana na mchezo wenyewe, kocha lazima aangalie kikosi alicho nacho ndipo anapanga wachezaji, wala hakuna kiongozi ambaye anaweza kumuingilia kocha kupanga kikosi.
“Hata kama ungekuwa na kikosi kizuri namna gani, hakuna timu ambayo kila mechi lazima itashinda, suala la mashabiki kulaumu ni la kawaida. Omog ameangalia mashabiki wana kiu ya ubingwa hivyo anatumia mfumio ambao utampa matokeo kulingana na wachezaji waliopo,” alisema Manara.
Aidha Manara amesisitiza kuwa klabu yake haitamuondoa Omog kwani anafanya vizuri na wana uhakika wataibuka washindi kwenye mashindano yote yaliyoko mbele yao.
No comments:
Post a Comment