CONTE: MORATA NINAWEZA KUMPA BINTI WANGU. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Sunday 24 September 2017

CONTE: MORATA NINAWEZA KUMPA BINTI WANGU.

KOCHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Antonio Conte, amemmwagia sifa mshambuliaji wake, Alvaro Morata, huku akidai kuwa ana nidhamu ya hali ya juu na angeweza kumpa nafasi ya kumuoa mtoto wake.

Hata hivyo, kocha huyo amesisitiza kuwa yupo kwenye mipango ya kumfanya mchezaji huyo aendelee kuwa bora zaidi na nidhamu ya hali ya juu.

Mchezaji huyo amejiunga na Chelsea katika kipindi hiki cha majira ya joto akitokea Real Madrid kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Diego Costa ambaye tayari yupo nchini Hispania kwa ajili ya kujiunga na klabu yake ya zamani, Atletico Madrid.

“Nimekuwa nikimjua Morata kwa kipindi kirefu sana, ukweli ni kwamba mchezaji huyo ana nidhamu ya hali ya juu, nadhani Chelsea imefanya maamuzi sahihi ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24.

“Naweza kusema ninampenda mchezaji huyo kwa kuwa amekamilika kwa kiasi kikubwa na anaweza kubadilika kutokana na mazingira yaliyopo.

“Tabia yake akiwa mazoezini inafaa kuigwa na kila mchezaji, mchezaji mwenye upole wa hali ya juu na nampenda kwa kuwa ni mmaliziaji mzuri, kutokana na hali hiyo, unaweza kumpa mtoto wako akamuoa, hata kwa upande wangu ningeweza kumpa mwanangu, lakini tayari ana mke wake,” alisema Conte.
Conte amedai kuwa uwepo wa Morata ndani ya kikosi hicho utaweza kuziba nafasi ya Costa, hivyo hana wasiwasi na kuondoka kwake.

“Napenda kumshukuru Costa kwa mchango wake katika kipindi chote ambacho tulikuwa pamoja, tuliweza kutwaa taji tukiwa wote, hivyo ninajivunia kuwa na mchezaji kama huyo kwenye kikosi kwa kuwa amekuwa miongoni mwa historia ya Chelsea.

“Napenda kumtakia kila la heri huko aendako na ninaamini ataendelea kufanya vizuri zaidi ya hapa, sikuwa na tatizo na mchezaji huyo na tunaweza kushikana mikono popote nitakapokutana naye.

“Hata hivyo, siwezi kuzungumzia sana mambo ya Costa kwa kuwa si tena mchezaji wa Chelsea, lakini naomba niweke wazi kuwa kila mchezaji msimu uliopita alikuwa muhimu kwenye kikosi na ndio maana tulichukua ubingwa na si kwa sababu ya fulani, hii ni timu,” aliongeza.

Kwa upande wa Morata tangu ajiunge na kikosi hicho cha mabingwa watetezi amefanikiwa kufunga mabao matatu huku akitoa pasi mbili za mwisho katika michezo minne aliyoanza kabla ya mchezo wa jana.

No comments:

Post a Comment