Katibu wa Baraza la Wazee wa Klabu ya Yanga, Ibrahimu Akilimali maarufu kama Abrahmovich ameibuka na kusema kuwa kikwazo kikubwa kwa Yanga kutochukua ubingwa msimu huu wa 2017/2018 ni makamu mwenyekiti Clement Sanga.
Akizungumza Mzee Akilimali amedai kuwa hata mgomo uliotokea juzi tarehe 19 Septemba wa wachezaji kugomea mazoezi ni njama iliyopangwa na Sanga.
“Baada ya wachezaji kutoka kumuona mwenyekiti wetu, Yusuf Manji kesho yake tunaskia kuwa timu imegoma kufanya mazoezi halafu hapo hapo anakutwa Clement Sanga mazoezini akiwa na kamusoko na Canavaro wakiwa wanateta, ile Sanga kuondoka tu mazoezini timu imegoma,” alisema Mzee Akilimali
Aidha Mzee Akilimali amemtaka Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo Clement Sanga kujiuzulu kwa madai kuwa yeye ndiye chanzo cha matatizo yote yanayotokea ndani ya Klabu hiyo.
“Nawasihi Watanzania wote hususani wana Yanga na wapenzi wa Yanga kuwa Sanga sasa hivi atamke kujiuzulu, chonde chonde Bwana Sanga iache Yanga watu tuketi pamoja na wewe mwenyewe tuchague viongozi Yanga tusonge mbele” amesema Mzee Akilimali.
Hata hivyo wachezaji wa Yanga jana walimaliza mgomo wao na kufanya mazoezi kama ilivyokuwa kawaida yao kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Jumamosi dhidi ya Ndanda FC utakaopigwa kwenye dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment