TRA KUPIGA MNADA TANI 40 ZA SUKARI KILIMANJARO - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday 3 April 2018

TRA KUPIGA MNADA TANI 40 ZA SUKARI KILIMANJARO

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, imesema itauza sukari ambayo ilikuwa ikiingizwa nchini kwa njia ya panya kutoka Kenya.
TRA ilikamata bidhaa mbalimbali ikiwamo zaidi ya tani 41 za sukari na lita 27,000 za mafuta ya taa yaliyoingia nchini kupitia njia zisizo rasmi kutokea Kenya.
Bidhaa nyingine zilizokamatwa ni chumvi katoni 2,000, bidhaa ndogondogo za viwandani zikiwamo pipi katoni 397 na vyombo vya usafiri vilivyokuwa vikisafirisha bidhaa hizo pikipiki 52 pamoja na magari 17.
Meneja msaidizi wa forodha mkoani Kilimanjaro, Godfrey Kitundu alisema sukari hiyo ilikamatwa kati ya Desemba 2017 na Machi na kwamba, imezuiwa katika ofisi za mamlaka hiyo kusubiri kibali cha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ili iuzwe.
Kitundu alisema bidhaa nyingine zilizokamatwa tangu Julai 2017 hadi Machi na kwamba, baada ya kutozwa kodi na faini zimeiingizia mamlaka hiyo zaidi ya Sh368.7 milioni.
Alisema kumekuwapo na changamoto kubwa katika kudhibiti bidhaa zinazoingia na kutoka nchini, kutokana na kuwapo kwa njia za panya zaidi ya 300 ambazo hutumiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu. “Kilimanjaro tuna mipaka mikubwa mitatu ambayo mizigo inapaswa kupitia; kituo cha pamoja cha Forodha Holili, mpaka wa Tarakea na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (Kia), lakini kutokana na jiografia ya mkoa huu, kuna njia zaidi ya 300 za panya ambazo zinaenda Kenya, hili limesababisha changamoto kubwa katika kudhibiti uingizwaji bidhaa kinyume cha sheria,” alisema.
Pia, alisema njia za panya zimekuwa zikipitisha bidhaa kama sukari, mafuta ya taa, chumvi, maziwa, bidhaa za viwandani zikiwamo pipi na simu za mkononi na kwamba wameendelea kujipanga ili kudhibiti tatizo hilo.
“Bidhaa hizi zimekuwa zikipitishwa kwa wingi kwa kutumia pikipiki. Julai 2017 hadi sasa tumekamata pikipiki 52 na magari 17,” alisema Kitundu.
Alisema kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi, wameendelea na operesheni ili kutokomeza uingizwaji bidhaa za magendo na kwamba, zinazohusu chakula na dawa waliwasilisha sampuli TFDA ili kuthibitisha kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu.

No comments:

Post a Comment