Dar es Salaam. Sintofahamu iliyotokea Zimbabwe baada ya jeshi la nchi hiyo kutanda jijini Harare na kumuweka chini ya uangalizi Rais Robert Mugabe imeelezwa ni jambo jipya ambalo halijawahi kutokea.
Baada ya taarifa kusambaa kuwa jeshi linaidhibiti nchi hiyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa hapa nchini mbali ya kueleza kuwa ni jipya, pia wameeleza kuwa ung’ang’anizi wa madaraka ni tatizo.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu kilichotokea Zimbabwe, makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisema ni jambo jipya kuwahi kutokea katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi za Afrika zinafuata mfumo wa demokrasia wa kuchagua viongozi kupitia vyama.
Msekwa, ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema anasita kuita mapinduzi kutokana na kilichotokea Zimbabwe kwa kuwa mapinduzi ya kijeshi huhusisha kuitoa Serikali iliyopo madarakani kisha jeshi kushika hatamu, jambo ambalo kwa nchi hiyo wanajeshi wametangaza kuwa hawako tayari kukamata madaraka.
“Katika kumbukumbu zangu sikumbuki kama hili jambo limewahi kutokea tangu miaka ya 60, kuna tofauti kubwa sana kuita haya ni mapinduzi ya kijeshi. Ni mapinduzi kwa sababu Serikali iliyokuwepo imetolewa lakini jeshi limesema halina nia ya kuchukua madaraka, ni jambo jipya sana kwangu ndiyo maana nasita kuita ni mapinduzi ya kijeshi,” alisema.
Hata hivyo, kada huyo wa chama tawala alisema kila jambo lina mwanzo wake pengine na hilo limekuja kwa makusudi ili watu wajifunze.
Msekwa alilipongeza jeshi hilo kwa kuhakikisha wanafanya mambo hayo kwa amani bila kumwaga damu.
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema jambo lililofanyika nchini humo ni matokeo ya ung’ang’anizi wa madaraka, ingawa nyuma Mugabe alisukumwa na chama kilichokuwa kikitaka kiendeee kutawala milele. “Sasa tupo katika utawala wa kijamhuri unaotaka kuwe na uchaguzi huru, ukimuangalia Mugabe alishafika umri wa zaidi ya miaka 90 na bado alikuwa anang’ang’ania madaraka ndiyo maana amepata aibu,” alisema.
Profesa Mpangala alisema Mugabe angejiwekea heshima kubwa kama angekubali kung’atuka mapema na kuandaa vijana ambao wangemrithi na siyo mpaka kusubiri jeshi ‘limpindue’.
Alisema tukio hilo ni funzo kubwa kwa nchi mbalimbali kwa kuwa si kiongozi pekee anayeng’ang’ania madaraka anachokwa, lakini pia chama kiking’ang’ania nacho kinajiweka katika wakati mgumu.
“Ni lazima kuwe na mfumo wa kubadilishana madaraka, hiyo ndiyo demokrasia unayotaka na ni lazima Serikali iweke mazingira ya ushindani sawa kwa vyama vyote vya upinzani,” alisisitiza Profesa Mpangala.
Akizungumzia suala hilo, mratibu wa Mtandao wa Wapigania Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa alisema Rais Mugabe amejitengenezea mwenyewe mazingira hayo.
“Kilichotokea ni matokeo ya kutoheshimu demokrasia, alikuwa na muda wa kutoka kwa heshima na kuandaa watakaomrithi lakini ameshindwa hilo na matokeo yake akafanya chama ni mali ya familia,” alisema.
Ole Ngurumwa alipongeza hatua hiyo na kusema kuwa ilifika wakati wake na kuwa wananchi walishachoshwa na kiongozi huyo ambaye alianza kuongoza mara tu baada ya uhuru wa nchi hiyo kupatikana kutoka kwa wakoloni wa Uingereza.
Hata hivyo, Ole Ngurumwa alilipongeza jeshi hilo kwa kitendo chake cha kutomwaga damu na kusababisha maafa kwa wananchi.
“Wakati mwingine tunashuhudia damu ikimwagika bila sababu za msingi, tunashukuru jeshi la Zimbabwe limefuata njia bora ya demokrasia ambayo haimwagi damu na kuheshimu watu,” alisisitiza Ole Ngurumwa
No comments:
Post a Comment