POLISI YATOA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MASOGANGE - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Monday, 30 April 2018

POLISI YATOA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MASOGANGE

WAKATI kukiwa na shauku kubwa ya kujua sababu za mwili wa marehemu Agness Gerald ‘Masogange’ kufanyiwa uchunguzi wa kipolisi wakati ukiwa Mochwari ya Hospitali ya Muhimbili, Jeshi hilo limefunguka na kutoa ufafanuzi, huku likiwataka Watanzania kuelewa kuwa kufanyia maiti uchunguzi wa kipolisi ni jambo la kawaida.
UCHUNGUZI WA MUHIMBILI
Masogange (28) alifariki dunia Aprili 21, mwaka huu katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge jijini Dar na mwili wake kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Baadaye Polisi walifika hospitalini hapo na kuufanyia uchunguzi mwili huo hivyo baadhi ya watu waliowasiliana na gazeti hili walikuwa na shauku ya kupata ripoti ya uchunguzi huo.
KIFO CHENYE UTATA?
Kitendo cha Polisi kuufanyia uchunguzi mwili huo kilizua gumzo kwa baadhi ya watu waliofika hospitalini hapo, huku wengi wakihoji mantiki yake, wakiamini kuwa uchunguzi wa maiti hufanyika kwa watu waliokufa vifo vyenye utata.
“Inakuwaje Polisi wanachunguza mwili wa mtu aliyefariki dunia katika mazingira ya kawaida kabisa na hata ripoti za madaktari zinaeleza kuwa kifo hicho hakina utata?” Walisikika baadhi ya watu wakihojiana wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo, ikiwa sasa zimekatika takribani siku kumi tangu kifo hicho, Polisi ilikuwa haijaweka wazi matokeo ya uchunguzi huo, jambo ambalo limekuwa likiendelea kuzua mjadala mitaani kiasi cha baadhi ya watu kuanza kuhusisha tukio la kupimwa maiti yake na maisha ya marehemu enzi za uhai wake.
KAMANDA ATOA UFAFANUZI
Kufuatia sakata hilo, Ijumaa Wikienda liliamua kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Muliro Jumanne na kumwomba atolee ufafanuzi suala hilo ambapo mazungumzo hayo yalikuwa hivi;
Ijumaa Wikienda: Kamanda habari za kazi? Wakati mwili wa marehemu Masogange ukiwa Muhimbili, kulizuka taharuki baada ya Polisi kuuchukua mwili huo na kwenda kuufanyia uchunguzi. Watu walikuwa wakitamani kujua kwa nini ilikuwa lazima afanyiwe uchunguzi wakati tayari madaktari walieleza kuwa kifo chake ni cha kawaida?
Kamanda Muliro: Mimi naendelea vizuri. Lakini kwa nini iwe ni kifo cha Masogange, wakati suala la kufanyia uchunguzi maiti hufanywa kwa kila mtu? Ukienda pale Muhimbili wakati wote utakuta Polisi wapo wanafanya uchunguzi wa maiti.
Ijumaa Wikienda: Watu wanahoji kwa Masogange kwa sababu wanaamini kuwa kifo chake hakikuwa cha utata. Madaktari walishasema kuwa alikufa kifo cha kawaida, kwa nini afanyiwe tena uchunguzi wakati ripoti ya kifo chake ipo?
Kamanda Muliro: Nasema hiyo ni kazi ya Polisi siku zote. Kifo chochote kinatakiwa kufanyiwa uchunguzi, lakini sasa ninyi (Waandishi) macho yenu yako kwa mastaa tu. Polisi tunafanya uchunguzi hata kwenye vifo ambavyo tunajua kuwa kimetokana na nini.
“Tunachunguza hata waliokufa kwa ajali za pikipiki. Ni utendaji wa kawaida wa Polisi.
Ijumaa Wikienda: Sawa Kamanda nimekuelewa. Lakini sasa matokeo ya vipimo vya uchunguzi wa Masogange yameonesha nini?
Kamanda Muliro: Wewe chukua haya niliyokueleza kama ndiyo habari yako, kuhusu matokeo ya Masogange, hilo achana nalo. Natamani watu wangeelimishwa kwamba Polisi kuchunguza maiti ni suala la kawaida.
TUJIKUMBUSHE
Masogange aliyefariki dunia Aprili 21, mwaka huu katika Hospitali ya Mama Ngoma jijini Dar, aliagwa katika Viwanja vya Leaders vilivyoko Kinondoni Aprili 23 na kuzikwa nyumbani kwao katika Wilaya ya Mbalizi mkoani Mbeya Aprili 24.

No comments:

Post a Comment