FLAVIANA Matata ni miongoni mwa wanamitindo maarufu wa Tanzania duniani. Mwaka 2013, Jarida la Fobes la Africa liliandika kwamba ni miongoni mwa wanamitindo saba ambao wanaingiza kipato kikubwa Afrika.
Kama hiyo haitoshi, mwaka jana aliandikwa na mtandao maarufu duniani wa okay. com, kuwa ni miongoni mwa wanawake 100, wenye ushawishi zaidi barani Afrika, lakini pia mwanadada huyu mwenye urembo wa kipekee amefanikiwa kupamba majarida mengi likiwemo New African Woman (2015). Zaidi, Flaviana ni mjasiriamali, anamiliki bidhaa zenye Lebo ya Lavy ambazo ni rangi za kupaka kucha za mkononi, anafanya kazi za jamii pia, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha mabinti wadogo kuhusu elimu, kupambana na kuamini kupitia vipaji vyao.
Haya anayafanya chini ya taasisi yake iitwayo Flaviana Matata Foundation, pamoja na ‘project’ mbalimbali kutoka kwenye makampuni tofautitofauti.Huyo ndiye Flaviana Matata, mwanamke wa chuma ambaye ukurasa huu umekuletea uweze kuona alivyokataa kushindwa na kupambana kuitafuta heshima aliyonayo leo katika maisha yake hasa kupitia kile alichokiamini, yaani mitindo.
MAISHA YAKE YA UTOTO
yangeweza kumkatisha tamaa! Suala la watu wengi kupoteza ndoto zao kutokana na changamoto za utotoni si ngeni. Kuna msemo unasema kwamba mustakabali wa maisha ya mtu ni vile anavyolelewa na kukua wakati akiwa mtoto. Kwa Flaviana, maisha ya utotoni pengine ni kama ambayo wamepitia watu wengi, yenye kujaa changamoto. Akiwa binti mdogo alimpoteza mama yake katika ajali ya meli ya MV Bukoba, mwaka 1996.
Hilo lilikuwa pigo kubwa kwake na lilisababisha alelewe na baba yake pekee. Lakini kumkosa mama yake, ingawa ilikuwa ni hali iliyojaa machungu kila siku, lakini hakurudi nyuma, alisonga mbele akikua katika imani ya siku moja kufanikiwa kwenye maisha yake.
ALIKUWA ‘TOM BOY’
Mwaka 2014, katika ‘project’ yake na Malaria No More, Flaviana Matata aliwahi kueleza kwamba wakati wa utoto alikuwa ‘tom boy’, kwa maana kwamba alikuwa anapenda kucheza michezo ya kiume, hasa mchezo wa mpira wa miguu.Kwa watu wengi, kwa wakatio huo, msichana kucheza mpira wa miguu pengine lingeonekana kwamba ni tatizo, lakini kwake michezo ilikuwa ikimsaidia katika afya, kukua vizuri kiakili na kushirikiana na watoto wenzake katika michezo.
Kwa upande wa darasani, Flaviana alikuwa akipenda sana masomo ya sayansi. Na ndoto yake ya kuwa ‘engineer’ aliifanikisha katika Chuo cha Arusha Technical Collage (ATC), kabla ya kuingia kwenye mambo ya umiss mwaka 2007.Sasa jiulize, injinia kuanza mambo ya umiss na mitindo? Lingekuwa jambo la kuwashangaza wengi. Lakini Flaviana, kama mwanamke wa chuma aliweka vyeti vyake pembeni na kuianza safari mpya ya mafaniko kupitia kipaji chake!
ILIKUWA RAHISI KUTOBOA!
Wengine wanaweza kufikiri hivyo. Kwamba ilikuwa rahisi kutoboa kwa Flaviana aliyezaliwa mkoani Shinyanga na kupata mafanikio hayo aliyonayo. Lakini hakika haikuwa hivyo. Flaviana, katika mahojiano mbalimbali ambayo amefanya na vyombo vya habari amewahi kuweka wazi kwamba, haikuwa rahisi kufanikiwa, kuna wakati alikutana na changamoto kama ambavyo watu wengi wamekutana nazo.
Flaviana amewahi kuzungumza na Mtangazaji Salama Jabir, kwenye Kipindi cha Mkasi kwamba, hata kazi yake ya kwanza aliyofanya na Kampuni la TIGI ya London, Uingereza kutangaza nywele haikuweza kutoka. Kwa mtu anayeanza kupambania ndoto zake, hali kama hii ingeweza kumkatisha tamaa. Lakini haikuwa kwake, alikaza buti na leo ana heshima kubwa duniani.
KUHUSU MAFANIKIO ANASEMAJE?
Kuhusu mafanikio Flaviana Matata, ambaye kwa sasa anafanya kazi na Kampuni za The Lions ya Marekani, Next Model Management ya Ufaransa na Uingereza, Sight Management Studio ya Hispania na Boss Models ya Afrika Kusini, mara kwa mara huwaambia mabinti wanaohitaji kupambana kufikia ndoto zao kwamba: “Hakuna aliyesema itakuwa rahisi. Bakia kwenye kile unachokiamini, fanya kazi kwa bidii na kuwa mnyenyekevu.
No comments:
Post a Comment