TAIFA STARS KUONA MAKALI YA CONGO. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday, 27 March 2018

TAIFA STARS KUONA MAKALI YA CONGO.

Wakati nchi nyingi zikitumia mechi za kirafiki kwa maandalizi au kupima ubora wa vikosi, Tanzania inatumia michezo hiyo kujenga timu ‘imara’.
Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ leo inajitupa uwanjani kumenyana na DR Congo, katika mchezo wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Taifa Stars inayonolewa na Salum Mayanga, ilichapwa mabao 4-1 na Algeria mjini Algiers katika mchezo wa awali wa kalenda ya Fifa Machi 24.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Selemani ‘Morocco’ alisema kucheza michezo miwili na timu ngumu za Algeria na DR Congo kuna maana kubwa kwa kikosi hicho.
“Ninafikiri tunaanza kujenga timu mpya na mechi hizi zinatusaidia, kwasababu tunacheza na timu zilizojiandaa vizuri ambazo zimetuzidi kiwango. Nina matumaini baada ya muda mfupi timu itakuwa bora na itafanya vizuri zaidi.
“Jambo la msingi ni mashabiki kujitokeza kutuunga mkono na kutushangilia kwasababu sapoti yao ndio itatupa hamasa ya kufanya vizuri,” alisema Morocco.
Morocco alidai benchi la ufundi limefanyia kazi kasoro zilizojitokeza dhidi ya Algeria na sura mpya zinaweza kuanza katika mchezo wa leo ili kuwapa uzoefu.
Kocha huyo alisema mkakati ni kutoa fursa kwa wachezaji chipukizi kuonyesha vipaji na kuwajengea uwezo wa kujiamini katika michezo yenye ushindani.
“Ingawa mechi za kirafiki ni ngumu, lakini hatuwezi kubadili kikosi chote, kwenye mchezo dhidi ya DRC tutatoa nafasi kwa baadhi ya wachezaji vijana,” alisema.
Kocha wa DRC, Florent Ibenge alisema atawapa nafasi nyota wake wote wanaocheza soka la kulipwa Ulaya na ameahidi ushindi katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment