Mwigulu Nchemba aliamsha dude Jangwani - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Monday, 8 January 2018

Mwigulu Nchemba aliamsha dude Jangwani

NDIVYO unavyoweza kusema. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ni mnazi mkubwa wa Yanga, Mwigulu Nchemba, ameliamsha dude Jangwani.

Ndio, ni baada ya juzi Jumapili wanachama wa Yanga kuvimba kwa hasira ya kutaka kummeza mtu baada ya mkutano wao wa viongozi wa matawi kuzuiwa, serikali kupitia wizara hiyo ya Waziri Nchemba imeridhia kufanyika kwa mkutano huo na ikitoa pia ulinzi mzito.

Iko hivi. Jumapili asubuhi viongozi wa matawi wa Yanga waliitana klabu kwao ili kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni mchakato wa mkutano mkuu wa kuridhia mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu yao uliopangwa kufanyika Januari hii, lakini ghafla walivamiwa na askari Polisi na kuvunjiliwa mbali.

Askari hao walidai walidokezwa na mnoko mmoja kuwa mkutano huo ulikuwa na nia ya kuzusha vurugu na kuhatarisha amani klabuni hapo, jambo ambalo halikuwa kweli.

Baada ya zuio hilo uongozi wa Yanga uliwasiliana na jeshi la Polisi na haraka taarifa hizo zilimfikia Waziri Nchemba, aliyejiridhisha kabla ya kutoa maagizo ya kutolewa kwa kibali cha si tu mkutano huo uendele, bali mikutano ya klabu hiyo ifanyike.

Katika kibali hicho ambacho Mwanaspoti imeonyeshwa, Mwigulu alienda mbali zaidi akitaka polisi kutoa ulinzi wa kutosha katika mikutano hiyo, ili kama watatokea wa kufanya fujo wakamatwe na kushughulikiwa na jeshi hilo.

Hatua hiyo ikaenda mbali zaidi ambapo jana Jumatatu mchana Yanga kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wake, Boniface Mkwasa, ambaye ndiye aliyemuandikia barua Waziri Nchemba, walipokea barua rasmi kutoka kwa Katibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Nelson Kaminyonge wakipewa ruksa ya kufanyika kwa mikutano yao.

Aidha Kaminyonge amewataka Yanga kuhakikisha wanafanya mikutano hiyo kwa kuzingatia amani na utulivu huku wakitakiwa kujadiliana mambo ya maendeleo ya klabu yao hatua ambayo imepokewa kwa furaha na wanachama wa Yanga.

Akizungumzia hatua hiyo, Mratibu wa mkutano huo, Edwin Kaisi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tawi la Uhuru, alisema wamepokea kwa furaha maelekezo hayo.

“Siku zote Yanga tunaheshimu mamlaka hususani serikali, kama utaona jana (juzi) tulivyozuiwa tusifanye mkutano hatua iliyotuumiza ila tulikubaliana isitokee vurugu na sasa tutafuata taratibu kuitisha tena mkutano wetu,” alisema Kaisi.
“Sisi Yanga si watu wa vurugu.”

No comments:

Post a Comment