Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa ameshusha presha ya kocha wake George Lwandamina baada ya kupona sawasawa majeraha yake ya mguu aliyoyapata katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar.
Mshambuliaji huyo wikiendi iliyopita alifunga bao moja na kutengeneza moja wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Kagera Sugar ameonekana jana akifanya mazoezi vyema akipambana kwa nguvu na mabeki wa timu hiyo.
Hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa jana ambapo alionekana kucheza huku akiwa na maumivu huku akikwepa kupambana kwa nguvu na wenzake baada ya kuumia katika mchezo uliopita ambao alitolewa dakika za mwisho.
Hatua hiyo imemfanya Lwandamina kuondoa wasiwasi wa kumkosa mshambuliaji huyo akisema kwa sasa wako sawasawa na hakuna majeruhi yoyote baada ya kupona kwa Chirwa.
"Tulipata wasiwasi jana alipokuwa akichechemea, lakini kama ulivyoona madaktari walipambana na sasa amekuwa sawa tunahitaji kuwa na wachezaji wetu wote kuelekea mchezo ujao kwa hiyo kupona kwake ni faraja kwa timu," alisema Lwandamina.
Katika hatua nyingine, Yanga imewasafirisha wachezaji wake watano walioachwa awali jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuongeza nguvu kuelekea mchezo dhidi ya Stand United.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema amewapokea wachezaji wake watano ambao awali waliachwwa katika safari ya kuelekea Bukoba baada ya kukosa nafasi katika ndege.
Hafidh amewataja wachezaji hao kuwa ni kipa kinda Ramadhan Kabwili, mabeki Pato Ngonyani, Abdallah Haji 'Ninja'na viungo Said Mussa na Juma Mahadh.
Alisema wachezaji wao watatu washambuliaji Donald Ngoma, Amissi Tambwe na kiungo Thabani Kamusoko ambao wanahudhuria kliniki maalum wataungana na timu hiyo mara baada ya mchezo wao dhidi ya Stand United.
No comments:
Post a Comment