Waziri Mkuu:Katiba Mpya bado - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday 9 November 2017

Waziri Mkuu:Katiba Mpya bado

DODOMA. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua mchakato wa Katiba mpya, lakini kwa sasa kipaumbele chake ni kuwapa wananchi huduma za jamii.

Akijibu swali la Mbunge wa Temeke (CUF), Abdalla Mtolea katika maswali ya papo kwa papo bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi, Majaliwa alisema kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwapa huduma za jamii wananchi ili waendelee kufanya kazi zao za kuboresha uchumi wao.

“Ni kweli serikali ya Awamu ya Nne ilianza mchakato wa katiba mpya na kupitia hatua zote za kuunda tume, kukusanya maoni na sisi kama wabunge tulikuwa miongoni mwa wajumbe ambao tulishiriki katika kuweka misingi nya katiba hiyo,” alisema Majaliwa.

Alisisitiza kuwa suala la katiba mpya linahitaji gharama kubwa ya fedha ambazo hutokana na mapato yanayokusanywa ndani ya nchi na kwamba kila mwaka wa fedha kuna vipaumbele vyake, lakini kwa sasa Serikali imejitika kutoa huduma za jamii kwa wananchi kwanza.

“Tumekuwa tukishuhudia Watanzania wakihitaji maji kwenye vijiji, kumekuwa na mahitaj ya huduma za jamii za afya, tunahitaji kuimarisha elimu, miundombinu ili kuwawezesha kuendeleaa na maisha yao,” alisema na kuongeza;
“Katiba ni muongozo unaooweza kuwaongoza, ni muongozo ambao unaelekeza mambo kadhaa. Sasa hivi tunayo katiba ambayo ina miongozo ileile ingawa tumekusudia kuibadilisha,” alisema Majaliwa.

Alisema kwa sababu katiba ya sasa nayo inatoa muongozo huku ikihitaji marekebisho katika maeneo kadhaa na kwa sababu mchakato wake unahitaji gharama kubwa,itaendelea kutumika mpaka hapo Serikali itakapofikia hatua nzuri ya mapato na kupunguza matatizo ya wananchi.

“Matatizo hayo yakipunguza kwa kiasi kikubwa tutakuja kuendesha mchakato huu pale ambao inaonekana tunaweza kuufanyia kazi,” alisema.

Awali, mbunge wa Temeke alitaka kujua hatua ambazo serikali ya Awamu ya Tano imefikia katika kushughulikia mchakato wa Katiba mpya ambao ulianzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne na kutumia fedha nyingi.

No comments:

Post a Comment