Muingiliano wa madaraka katika klabu kongwe Simba na Yanga, umetajwa kuwa ni chanzo cha makocha na wachezaji kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu kama lilivyozungumzwa na wadau wa soka nchini.
Kocha wa Azam B, Abdul Mingange ambaye ni meja mstafu wa jeshi, alisema inashangaza kuona viongozi wa klabu hizo wanazungumzia viwango vya wachezaji pamoja na afya zao kitu ambacho si sahihi.
"Hakuna kitu kilichoshangaza kiongozi kuzungumzia suala la Shomary Kapombe, jambo ambalo alitakiwa kulizungumzia daktari, alitolee ufafanuzi kwa wanachama wao ambao wanahitaji kujua taarifa za mchezaji wao.
"Hii inasababisha kuharibu saikolojia za wachezaji pamoja na utendaji wa kocha ambaye pengine anaweza kumfikiria kwa mipango yake ya badaae,"
"Soka la Tanzania, linaendeshwa kijanjajanja kiasi kwamba hata usajili unafanywa na mashabiki na viongozi,mwisho wake wanampa mtihani kocha kushindwa kupanga kikosi chake, badala yake wao ndio wanapanga watu wao na kuwaacha wanaojua nje,"alisema.
Mingange alisema wanafikia hatua ya kushindwa kusajili mahitaji, badala yake wanajaza watu kwenye klabu ambao wana manufaa nao.
Kocha wa zamani wa Toto Africans, John Tegete alisema hilo ni janga la taifa, kwa madai kuwa muingiliano wa madaraka na ujuaji unadhoofisha maendeleo ya soka.
"Yaani kisichoingiliwa kwenye soka labda ni mchezaji afanyiwe upasuaji hapo hawawezi kuongelea kiundani kwani ni mambo ya sayansi, ifikie hatua kila mtu asimame kwenye wajibu wake, waache haya mambo ya ujuaji wa kila jambo."
"Kocha Arsene Wenger anabezwa na wengi, lakini anaendesha soka kisasa ameajiri mtu wa kufuatilia wachezaji wa kuwasajili kama wanafaa kuingia kwenye klabu au la, siyo Yanga na Simba ambao viongozi wao ndio kila kitu, mwisho wa siku yanawashinda,"
"Tubadilike kinachotakiwa ni benchi la ufundi lipewe nguvu,hapo mambo yanaweza kusonga mbele lasivyo kila mtu akijifanya anajua soka ni hatari na mwisho wake ndio huo kuwalalamikia wachezaji, kwani wakati wanawasajili hawakuwachunguza,"alihoji.
Naye kocha wa zamani wa Njombe Mji, Hassan Banyai alisema kiongozi anapaswa kuzungumzia kiwango ama afya ya mchezaji kwa ripoti maalumu kutoka kwa daktari ama kocha.
"Viongozi wajifunze mbona makocha hawawezi kuzungumzia suala la uongozi!ifikie hatua waache mambo ya kizamani ambayo mwenyekiti yeye ndiye anashika pesa, anapanga kikosi,anasajili,yaani kila kitu yeye huo siyo mpango,"alisema.
No comments:
Post a Comment