Omog nje simba SC,Matola atajwa - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday 31 October 2017

Omog nje simba SC,Matola atajwa

Pamoja na kuwa na rekodi ya kutofungwa na Yanga, kocha wa Simba, Mcameroon Joseph Omog siku zake ndani ya klabu hiyo zinahesabika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo zinadai kuwa mechi ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Yanga ulikuwa mtihani wa mwisho kwa kocha Omog.

Sare ya bao 1-1 iliyopata Simba dhidi ya Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa ni sare tatu kwa Omog tangu atue nchini matokeo ambayo vigogo wa klabu hiyo hawakupenda.

Chanzo hicho kilidai kuwa Omog kilichokuwa kimemuweka Simba hadi sasa ni mechi dhidi ya Yanga pamoja na taratibu za vibali vya kazi vya kocha Masoud Djuma.

Imeelezwa ndani ya Simba kulikuwa na majadiliano yaliyokuwa yanaendelea juu ya kocha msaidizi ambapo mapendekezo ni kupata kocha msaidizi mzawa na jina lililokuwa limependekezwa ni la Seleman Matola anayefundisha Lipuli FC.

"Ni mambo ambayo yapo ndani ya Simba kwasasa ingawa bado majadiliano kuhusu kocha msaidizi yalikuwa yanaendelea kwani anayetakiwa kwasasa ni kocha mzawa ni muda tu unasubiriwa kuhusu kuondoka kwa Omog na Djuma apewe majukumu hayo, " alisema mjumbe huyo wa Kamati ya Simba.

Omog mpaka sasa amewahi kucheza mechi nane dhidi ya Yanga na kati ya hizo tatu alimaliza akiwa na wachezaji pungufu lakini hakupoteza.

Kocha huyo raia wa Cameroon amewahi kuinoa Azam na sasa Simba. Akiwa Azam alicheza dhidi ya Yanga mara tatu, na kupoteza mchezo mmoja tu.

Mechi ya kwanza ilikuwa Machi 2014 ambapo aliyekuwa beki wa Azam, Erasto Nyoni alionyeshwa kadi nyekundu wakati huo Yanga ikiongoza bao 1-0 lakini Kelvin Friday alisawazisha dakika za mwishoni na kufanya mchezo huo kumalizika 1-1.

Mechi nyingine ilikuwa ya Ngao ya Hisani Agosti 2014 ambapo alipoteza 3-0 kabla ya kupata sare ya 2-2 Desemba mwaka huo.

Omog akiwa Simba amekutana na Yanga mara tano na mbili kati ya hizo alimaliza akiwa na mchezaji mmoja pungufu, lakini hakupoteza.

Pigo la kwanza kwa Omog lilikuwa Oktoba mwaka jana ambapo Jonas Mkude alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 26 wakati huo Simba ikiwa nyuma kwa bao moja, lakini Shiza Kichuya aliisawazishia Simba dakika za mwishoni na mchezo kumalizika 1-1.

Omog alishuhudia timu yake pia ikicheza pungufu Februari mwaka huu baada ya Janvier Bokungu kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 55, wakati huo Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0 lakini mabao kutoka kwa Kichuya na Laudit Mavugo yalitosha kuipa Simba ushindi wa 2-1.

Hivi karibuni, Simba ilivunja mkataba na kocha wake msaidizi Mganda Jackson Mayanja aliyedai ana matatizo ya kifamilia hivyo anakwenda kushughulikia matatizo hayo na atakosa muda wa kuwa karibu na kikosi cha Simba.

Hata hivyo, siku moja baada ya Mayanja kuondoka Simba walileta kocha mwingine Mrundi, Djuma aliyekuwa anaifundisha Rayon Sport ya Rwanda.

Habari ambazo zimepatikana ni kwamba Djuma hakuamini mkataba na Simba hadi baada ya mechi ya watani kumalizika kwani kilichokuwa kinasubiriwa ni kukamilisha kwa makubaliano yao ambayo ni kupewa ukocha mkuu wa timu hiyo.

No comments:

Post a Comment