Tshishimbi awagomea - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday 31 October 2017

Tshishimbi awagomea

KIUNGO wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi amekiri kwamba Aishi Manula wa Simba ni bonge la kipa na Msimbazi washukuru Mungu. Lakini, akasisitiza kuwa alipambana kiume dakika zote kugomea Simba isiwadhibiti wala kushinda ili kulinda heshima ya klabu na mashabiki wa Yanga.

Mchezaji huyo alidokeza pia kwamba dakika 15 za kwanza zilimtosha kuwasoma na kudhibiti mbwembwe za viungo wa Simba kwenye mechi ya juzi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Akizungumza na Mwanaspoti jana jijini Dar es Salaam, Tshishimbi alisema kabla ya mchezo huo aliambiwa na kocha wake George Lwandamina juu ya mipango ya Simba kutaka kumpangia viungo wengi ndio maana akaingia uwanjani akiwa na uelewa wa kutosha tu.

“Tulipokuwa katika maandalizi ya mchezo kocha aliniambia juu ya Simba kuwa, ni imara katika kiungo na kutakuwa na watu maalumu kwa ajili yangu na nikaingia katika mchezo huo nikiwa na akili hiyo,” alisema Tshishimbi anayeishi Masaki, Dar es Salaam eneo wanalokaa vigogo wenye noti zao.

“Tulipoanza mchezo nilitumia dakika 15 tu kuwasoma viungo wao na kujua wana ubora wa aina gani kisha, nikatafuta akili ya ziada ili niweze kuwakabili na hapo ndipo nilipofanikiwa. Wao kazi yao walikuwa wamenikamia tu, hakuwakuwa na jipya kabisa.

“Unajua tangu nimekuja Tanzania hasa hapa Yanga kila mchezo umekuwa mgumu sana kwangu kutokana na viungo wengi kuingia uwanjani kwa nia ya kunizuia, lakini nimekuwa nikitafuta namna ya kuwakabili.

“Haikuwa kazi rahisi kufanya vizuri kama vile... kutokana na aina ya mechi yenyewe, ile ni mechi na presha inakuwa kubwa na mbaya zaidi presha ni kutoka kwa mashabiki na inawaingia wachezaji, lakini nimekuwa sitaki hicho kinitokee ndiyo maana watu wamekuwa wakiona nafanikiwa uwanjani.

“Yanga wachezaji wanaushirikiano mzuri na ndio maana tukaweza kuibana Simba,” alisisitiza mchezaji huyo mwenye rasta na kuongeza kwamba, aliwasoma Simba vizuri kwenye mechi ya kwanza aliyokutana nao ndio maana hakuwa na presha.

Akizungumzia nafasi ya ubingwa, Tshishimbi alisema; “Tunaweza kuwa bingwa lakini kuna mambo tunatakiwa kuyaweka sawa, kwanza tuendeleze kufunga mabao kama tulivyoanza sasa lakini pia sisi kama wachezaji hatutakiwi kubweteka kila mechi kwetu ni kitu kigumu.”

Amkubali Manula

Kuhusu mashuti yake mawili ya maana aliyopiga kwenye lango la Manula, ambayo yamekuwa yakisambaa kwenye mitandao ya kijamii alisema; “Nilijipanga kuwafunga Simba, lakini kipa wao (Aishi Manula) aliwasaidia sana kuokoa, yule kipa mzuri. Lakini, bado nitaendelea kutafuta nafasi katika mechi zijazo.

“Mimi ni kiungo sio lazima nifunge, lakini kwanza huwa napenda kutengeneza nafasi kwa wenzangu wafunge na kama kunatokea nafasi ya kufunga naweza kufanya hivyo ndio maana nikawa najaribu mwenyewe kutokea mbali,” alisema.

Mwinyi amzungumzia

Naye beki wa kushoto wa Yanga, Mwinyi Haji alisema; “Ni mchezaji wa kiwango cha juu, yuko fiti na anacheza sehemu nyingi uwanjani. Anarudi kusaidia mabeki kukaba na pia anapanda kusaidia mashambulizi.”
“Ana vitu vingi adimu tofauti na viungo wengine, hii ndiyo sababu amemaliza unyonge wetu wa eneo la kiungo kwani, awali Simba walikuwa vizuri zaidi kwenye eneo hilo tofauti na sasa. Ana uzoefu mkubwa, pia kwenye mashindano ya kimataifa, akiendelea hivi atatubeba sana mwakani,” alisema.

No comments:

Post a Comment