Dar es salaam Mvua kubwa iliyonyesha wiki iliyopita jijini Dar es Salaam imeharibu miundombinu ya umeme.
Tathimini iliyofanywa na MTANZANIA kuhusu madhara yaliyosababishwa na mvua hiyo imeonyesha kuwa katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam miundombinu ya umeme ilisombwa na maji.
Maeneo yaliyobainika kukumbwa na uharibifu mkubwa ni Mbezi-Kimara, Mbezi chini na baadhi ya maeneo ya Magomeni.
Akizungumzia uharibifu huo jana, Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema amefanya ziara katika maeneo yaliyoathirika na kwamba tayari wahandisi wa shirika hilo wanayafanyia matengenezo.
Muhaji alisema eneo la Mbezi chini, darajani na kwa Malecela ndiyo yaliyoathirika zaidi lakini tayari kumefungwa nguzo na nyaya mpya.
Mhandisi Mkuu wa Tanesco wa Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Godlove Mathayo, alisema mafundi wanafanya jitihada kusimika nguzo na kushughulikia transfoma mbili zilizoharibika.
Alizitaja transfoma zilizoharibika kuwa moja iko eneo la Victoria na nyingine kwa Malecela.
“Baadhi ya transfoma zimezingirwa na madimbwi ya maji hivyo mafundi wameshindwa kuzifikia hadi maji yapungue.
“Baada ya matengenezo yanayoendelea sasa, wakazi wote wa maeneo ya kwa Malecela, Victoria na Kawe kwa maana ya eneo la Mbezi chini watapata huduma ya umeme kama kawaida,” alisema.
Wakati huo huo, Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Muhaji, jana aliwaomba radhi wateja wa shirika hilo walioathirika na ukosefu wa umeme katika maeneo yao.
“Lakini niwaombe tu wananchi watoe taarifa pale wanapoona maeneo yao hayana umeme watufahamishe ili mafundi wafike kwa haraka kufanya marekebisho, wanaweza kufanya hivyo kupitia anuani zetu na mitandao ya kijamii ya shirika,” alisema.
Akizungumzia kukatika kwa umeme katika eneo la Mbezi Temboni, kwa Msuguri, St. Anne na Kanisa la Udongo, alisema kulisababishwa na kulipuka kwa transfoma.
“Tunajua adha wanayoipata wananchi wa baadhi ya maeneo ya Mbezi Kimara ya kukosa umeme, baadhi ya transifoma zililipuka kwa sababu ya mvua na nguzo pia zilianguka.
“Lakini kwa sasa hali iko shwari, wamafundi wetu wanafanyakazi usiku na mchana kuhakikisha hakuna eneo linalokosa umeme nchini,” alisema Leila.
No comments:
Post a Comment