Uwezo mkubwa wa kuhakikisha lango lake linakuwa salama ulioonyeshwa na kipa wa Simba, Aishi Manula umemfanya kocha mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina ashindwe kujizuia na kusema kuwa kama siyo kipa huyo Simba walikuwa wanakufa.
Manula alifanya kazi kubwa ya kupangua michomo ya wachezaji wa Yanga katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, jambo ambalo liliiwezesha Simba kutoka sare ya bao 1-1 na mahasimu wao hao wa jadi hapa nchini.
Lwandamina alisema kuwa Simba wanapaswa kumshukuru sana Manula kutokana na umakini wake huo langoni kwani kama si yeye basi Yanga ingeondoka na pointi zote tatu katika mechi ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa.
“Mechi ilikuwa nzuri na yenye ushindani mkubwa lakini kikwazo kwa upande wetu alikuwa ni kipa wa Simba.
“Alifanya kazi kubwa sana ya kulinda lango lake, alikuwa makini sana na mahesabu yake yalikuwa makali, wachezaji wangu walijitahidi sana kadiri ya uwezo wao kupiga mashuti lakini aliyaona na kuyapangua kwa ufundi mkubwa, kwa hiyo nampongeza sana kwa hilo,” alisema Lwandamina.
Katika mechi hiyo, Manula ambaye amejiunga na Simba msimu huu akitokea Azam FC alipangua mashuti matano ya Yanga ambayo yalikuwa ya moto yaliyopigwa na Pappy Tshishimbi (mawili) Geofrey Mwashiuya, Emmanuel Martin pamoja Raphael Daudi.
Hata hivyo, akizungumzia kiwango chake hicho Manula alisema kuwa: “Hii ndiyo kazi yangu ambayo inanifanya nipate mkate wangu wa kila siku kwa hiyo ilikuwa ni lazima nifanye hivyo.
“Hata hivyo nichukue nafasi hii kuwaomba wapenzi na mashabiki wa Simba, wasife moyo kwa matokeo haya, nafasi ya kufanya vizuri ipo kwa hiyo waendelee kutuunga mkono tu.”
Manula mpaka sasa ameshafungwa mabao matano katika mechi nane za ligi kuu alizoitumikia Simba.
No comments:
Post a Comment