Mrundi wa Simba aanza kwa mikwara - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Thursday, 19 October 2017

Mrundi wa Simba aanza kwa mikwara

KOCHA msaidizi mpya wa Simba, Mrundi, Masudi Djuma ametua nchini jana na jambo la kwanza alilofanya wakati wa kutambulishwa ni kuchimba mikwara  mizito dhidi ya wapinzani wa Simba pamoja na wachezaji wa timu hiyo.

Masudi aliyeripotiwa jana kuwa anakuja nchini kuchukua nafasi ya Mganda Jackson Mayanja aliyetimka klabu hapo, alisema amekuja ili kuhakikisha Simba inasalia kileleni hadi mwisho wa msimu na kubeba ubingwa.

Lakini akafichua wazi kuwa, licha ya yeye kuwa mpole sana, lakini ni mkali mno kwa yeyote anayetaka kumvurugia kazi, na ni kama ujumbe anaupeleka kwa wachezaji wake kuwa, hatakuwa na mchezo kwa yeyote anatakayemzingua.

Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya mabao ikilingana pointi 12 na klabu za Yanga, Azam na Mtibwa Sugar na zote zikiwa zimecheza mechi sita kila mmoja, huku ikishikilia taji la Kombe la FA lililowapa uwakilishi wa mechi za kimataifa, mwakani ikicheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza kwenye utambulisho wake uliofanyika jijini Dar es Salaam, kocha huyo kijana na mwenye mbwembwe nyingi kama Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema hana mchezo katika kazi yake kwa sababu kiu yake ni mafanikio zaidi.

“Siwezi kukubali mtu achezee kazi yangu, kwani kwanza najua tunatafuta riziki lakini pia lazima timu iende mbele.” alisema kocha huyo aliyezaliwa Agosti 30, 1977 na kuichezea timu ya taifa lake la Burundi kati ya mwaka 1998-2006.

“Siwezi kuahidi kuwa nitafanya nini kwani kila kitu anapanga Mungu, hivyo namuomba aniwezeshe kutumia ujuzi wangu pamoja na ushirikiano na Kocha Mkuu kuifanya Simba iwe ya kwanza mpaka ubingwa mwisho wa msimu,”
“Sikuja kuleta maajabu ila nimekuja kusaidia kitu kidogo ambacho Mungu amenipa ili timu hii isonge mbele,” alisema Masudi.

Kocha huyo aliyezichezea klabu za Prince Louis, Rayon Sports na Inter Star kati ya mwaka 2002-2010 kabla ya kugeukia ukocha, alisema kuja kwake kuwa Kocha Msaidizi sio ajabu kwani Simba ni klabu kubwa na itakuwa kama shule kwake katika kusionga mbele kitaaluma.

“Watu wanaweza kushangaa Rwanda nilikuwa Kocha Mkuu, kisha huku nimekuja kuwa msadizi, lakini wajue nilianzia chini na baadaye nikasema nataka kupanda hivyo nikawa kocha mkuu, ila Simba nimekuja kusoma kwani ni klabu kubwa.”

MIAKA MIWILI

Kocha huyo ambaye mara baada ya kutambulishwa kwa wanahabari alikwenda kuonana na Kocha Mkuu, Joseph Omog, leo Ijumaa anatarajiwa kusainishwa mkataba wa miaka miwili ya kukinoa kikosi hicho chini ya Omog.

Chanzo makini ambacho Mwanaspoti inakiamini kinasema, mkataba huo utasainiwa mchana wa leo na kumpa jukumu la Mrundi huyo kuchukua mikoba ya Mayanja aliyeondoka klabu kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.

Simba inamsainisha Kocha Masudi aliyeibebesha ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda klabu ya Rayon Sports msimu uliopita kabla ya kujiuzulu, ikiwa ni wiki moja na ushei kabla ya kuvaana na Yanga katika mechi yao ya Ligi Kuu msimu huu.

MANARA

Akimtambulisha kocha huyo, Msemaji wa Simba Haji Manara amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kumpa ushirikiano kocha huyo, huku akitambulisha Meneja mpya Richard Robert anayechukua nafasi ya Dk Cosmas Kapinga aliyerejea kwa mwajiri wake kuendelea na kazi yake ya utabibu.

“Huyu ndiye kocha mmpya anayechukua nafasi ya Mayanja ambaye matatizo ya familia ndio yamemuondoa Simba na si kingine na tulimuomba atuvumilie hadi tutakapomalizana na kocha mwingine ndipo aondoke,” alisema Manara.

No comments:

Post a Comment