Jonas Mkude, kotei waliamsha dude Simba - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Friday 13 October 2017

Jonas Mkude, kotei waliamsha dude Simba

MITAANI kuna kelele nyingi kuhusu kiungo, Jonas Mkude, kutoanzishwa kikosi cha kwanza pale Simba, huku wengine wakiona poa kwa vile Mghana James Kotei anafanya vizuri kwenye eneo la kati.

Lakini huko mazoezini wameliamsha Kinachoendelea katika mazoezi ya Mnyama kuelekea mchezo wa keshokutwa Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar ni mpambano usio wa kawaida kati ya wachezaji hao wawili.

Viungo hao wamekuwa wakipambanishwa na kocha Joseph Omog, huku kila mmoja akionyesha vitu adimu ambavyo vimekuwa vikiwachanganya hadi wadau wa klabu hiyo kushindwa kujua nani mkali.

Katika tizi linalopigwa Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, kocha amekuwa akiwapa kazi viungo hao kuonyesha umahiri wao hasa kutokana na ugumu wa mechi hiyo ambayo Mtibwa wameonekana kuipania.

Katika mazoezi ya juzi Jumatano jioni, Omog aliamua kugawa timu yake katika vikosi viwili; cha kwanza kikiundwa na Aishi Manula, Ally Shomary, Jamal Mwambeleko, Yusuf Mlipili, Salim Mbonde, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Said Ndemla, Juma Liuzio, Nicholas Gyan na Haruna Niyonzima.

Huku kikosi kingine kikiwa na akina Emmanuel Mseja, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein, Method Mwanjali, Juuko Murshid, James Kotei, Jamal Mnyate, Mzamiru Yassin, John Bocco, Mohammed Ibrahim na Mwinyi Kazimoto.

Baada ya hapo akavipambanisha kwa muda wa dakika 40 na kazi kubwa ilionekana eneo la katikati kwa Mkude na Kotei kuonyeshana ushindani wa hali ya juu kila mmoja akitaka kumfunika mwenzake.

Wawili hao kila wakati walikuwa wakishindana katika kugombania mpira, kukaba na katika kuoneshana ufundi wa kupiga pasi ndefu na fupi jambo ambalo limeacha mtihani kwa kocha kwamba nani aanze.

Baada ya tizi hilo la nguvu, Omog aliliambia Mwanaspoti akisema: “Nimewaona vizuri walivyokuwa wanashindana, nami ndio dhumuni langu la kuwaweka timu mbili tofauti, nataka washindane na ambaye atakuwa vizuri zaidi ya mwenzake ndio atapata nafasi ya kucheza au kama watakuwa wapo vizuri wote basi nitawatumia wote kwani katika kikosi changu hakuna mwenye uhakika wa namba.”

Naye Mkude alipoulizwa ushindani wake na Kotei, alisema katika maisha ni lazima mtu akutane na changamoto, hivyo anachoangalia ni jinsi gani atafanya vizuri akiwa mazoezini au hata kwenye mechi ambazo atapata nafasi ili kumshawishi kocha awe anampanga kucheza mara kwa mara.

“Kotei ni mchezaji mzuri, kwa sasa ninachotakiwa ni kushindana naye mazoezini ili nionekane nipo vizuri zaidi yake na ndio maana kila wakati tunashindana akiwa na mpira yeye au mimi, yote hii nafanya kumshawishi kocha aweze kunipa nafasi,” alisema Mkude ambaye yeye na Kazimoto ndio wachezaji waliobaki katika kikosi cha Simba tangu walipochukua ubingwa wa mwisho wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011-2012.

“Kocha ndiye mwenye maamuzi ya mwisho ya yupi wa kumpanga au kumtumia, ila mimi nitatimiza yale majukumu yangu aliyonipa nikiwa uwanjani kwenye mazoezi au mechi.”

Mayanja, Mavugo wapishana

Daktari wa Simba, Yassin Gembe, amesema ukiwaondoa waliokuwa majeruhi ya muda mrefu, Said Mohammed ‘Nduda’ na Shomary Kapombe, hakuna mchezaji mwingine mwenye tatizo na vijana wapo tayari kwa mechi yao Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Hakuna majeruhi, lakini Kocha Msaidizi wetu Jackson Mayanja alienda kwao takribani wiki sasa, alikuwa na matatizo ya kifamilia ila atarajea kesho (leo) Ijumaa kuendelea na majukumu yake,” alisema.

“Pia mshambuliaji wetu Laudit Mavugo amekosekana katika mazoezi ya siku mbili kwa ruksa ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia ambayo yanamkabili na atarudi Jumamosi kuungana na wenzake.”

No comments:

Post a Comment