MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Alvaro Morata anatarajiwa kuwa nje ya uwanja si chini ya wiki sita baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja.
Morata alifanyiwa mabadiliko dakika ya 35 kwenye mchezo wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki dhidi ya Manchester City baada ya kuumia na nyota huyo ameachwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kinachojiandaa na mechi za kufuzu Kombe la dunia dhidi ya Albania siku ya Ijumaa na mchezo mwingine dhidi ya Israel siku ya Jumatatu.
Shirikisho la soka la Hispania limethibitisha kuwa kuwa kipimo cha MRI kimeonesha kuwa mshambuliaji huyo wa zamani ya Real Madrid na Juventus amepata jeraha la misuli ya paja na anatarajiwa kurudi mwezi Novemba.
Nyota huyo ambaye amesajiliwa kwa dau la rekodi ya klabu la Paundi milioni 70 ameshatupia magoli saba kwenye mechi kumi za mwanzo kwenye kikosi cha kocha Antonio Conte na anatarajiwa kukosa mechi za mwezi Oktoba pamoja na Novemba mwanzoni dhidi ya Crystal Palace, Manchester United, Watford na Bournemouth kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
Kukosekana kwa Morata kwenye kikosi cha Chelsea kunamfanya mbelgiji Michy Batshuayi kupata nafasi ya kuanza akiwa ndio mshambuliaji pekee aliyebaki kwenye kikosi cha Chelsea.
No comments:
Post a Comment