Afya ya lissu yazidi kuwa safii - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Monday 30 October 2017

Afya ya lissu yazidi kuwa safii

Alute Mughwai, kaka wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema afya ya mdogo wake imeimarika na anaendelea na mazoezi.

Mughwai alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi kuhusu maendeleo ya afya ya ndugu yake anayetibiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Lissu anatibiwa nchini humo baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma mchana wa Septemba 7, akitokea kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Kwa sasa nipo Arusha ila tangu nilipotoka hivi karibuni Nairobi alikuwa anaendelea vizuri na afya yake inaendelea kuimarika. Anaendelea na mazoezi kila siku, unajua chumba alichopo sasa ni kikubwa, kwa hiyo anafanya ndani humohumo,” alisema Mughwai.

Alisema Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) anapoonekana ametoka ndani kwenda nje ni kwa ajili ya kuota jua, lakini mara nyingi hufanya mazoezi ndani.

Tangu Septemba 7, Lissu hakuwahi kuonekana hadharani hadi Oktoba 18 zilipotolewa picha zake kwenye mitandao ya kijamii zikimwonyesha akiwa amelala kitandani na nyingine akiwa kwenye kiti cha magurudumu, huku akionekana mwenye tabasamu.

Mbali na picha, ujumbe wenye sauti ya Lissu uliorekodiwa ulisikika akiwashukuru Watanzania na watu wengine ndani na nje ya nchi. Alisema ni Mungu ndiye aliyeamua asife na si binadamu.

Kuhusu kusafirishwa nje ya Kenya kwa matibabu, Mughwai alisema kama alivyozungumza awali na gazeti hili, atafanya mkutano na waandishi wa habari kueleza masuala kadhaa likiwamo hilo.

Akizungumza na gazeti hili Oktoba 27, alisema wiki hii atafanya mkutano na wanahabari na anatarajia kueleza hatua inayofuata ya matibabu ya Lissu ambayo atayapata nje ya Kenya.

Oktoba 17, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema Lissu amefanyiwa upasuaji mara 17 na kuongezewa damu nyingi kuliko mgonjwa yeyote aliyewahi kulazwa katika Hospitali ya Nairobi kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Pia, Mbowe alisema baada ya matibabu ya awamu ya pili kukamilika, awamu ya tatu yatafanyika nje ya Kenya na kwa hatua hiyo, wataiachia familia kwa uamuzi na wao kama chama watakuwa nyuma ya wanafamilia kwa kila jambo watakaloamua.

No comments:

Post a Comment