SIMBA ilicheza soka safi. Simba ilimiliki mpira zaidi. Simba ilipiga pasi nyingi zaidi, lakini kwa bahati mbaya ama nzuri ilijikuta ikishambuliwa zaidi. Mambo yalikuwa kinyume.
Yanga haikuwa na umiliki mkubwa wa mpira, lakini ilikuwa na kasi katika mashambulizi. Ilijijenga kuanzia nyuma kwenda mbele. Ilitumia vizuri kasi ya washambuliaji wake; Obrey Chirwa, Pius Buswita na Geofrey Mwashiuya katika kulisakama lango la Simba.
Mwisho wa mechi Yanga ilikuwa imepiga mashuti tisa katika lango la Simba ikiwa ni matano zaidi ya yale ya wapinzani wao. Yanga ikatengeneza pia nafasi nyingi zaidi za kufunga. Kipindi cha kwanza chote Simba haikuwa na jaribio hata moja lililolenga lango.
Mara mbili wachezaji wa Yanga walibaki wenyewe na kipa wa Simba. Alianza Mwashiuya, lakini akakosa umakini na kupaisha mpira juu. Ndio wachezaji tuliojaliwa kuwa nao nchini. Akafuata Emmanuel Martins ambaye alishuhudia shuti lake likipanguliwa na kuwa kona. Nadhani mpaka sasa hafahamu kilichotokea.
Simba ilikosa ubunifu katika eneo la mwisho. Haikuwa na nguvu katika kupiga mashuti. Ilitegemea zaidi mipira ya krosi kutoka kwa Erasto Nyoni. Hata hivyo hilo halikuweza kuwa na madhara makubwa kwa wapinzani wao.
Ni Tshishimbi tena
Kuna wachezaji wa mechi kubwa na ndogo. Papy Kabamba Tshishimbi ni mchezaji wa mechi kubwa.
Amethibitisha hilo kwa mara nyingine tena. Amethibitisha mbele ya Simba tena baada ya kuwavuruga kabisa viungo wao.
Pamoja na kwamba Simba iliweza kumiliki mpira zaidi ya Yanga, bado Tshishimbi alionekana imara. Alitibua karibu kila mpango wa Simba. Kila walipotaka kwenda aliwarudisha.
Tshishimbi alikaba na kukaba tena Muda mwingi alikuwa injini ya timu na kuwapanga wachezaji wengine uwanjani. Alipanda pia kusaidia mashambulizi. Shuti lake la dakika ya 30 lilikuwa burudani zaidi. Hata Manula bado analikumbuka.
Kichuya yuko vizuri
Kuna wachezaji wana zali na mechi za watani. Shiza Kichuya ana zali tena kubwa kuliko lile la Mwanaspoti. Kichuya hakuhitaji kufanya kazi kubwa kuifunga tena Yanga. Alihitaji tu kuwa kwenye nafasi.
Mpira ulipigwa na Emmanuel Okwi, ukaguswa na kipa wa Yanga, Youthe Rostand, ukamkuta Mhenga Erasto Nyoni ambaye alimuona Kichuya akiwa amezubaa tu katika eneo la hatari na kumpa, akafunga kirahisi.
Maisha yanahitaji nini zaidi? Kichuya hakuhitaji kupiga shuti la umbali mrefu kama kwenye mechi zilizopita. Alihitaji tu kuwa katika nafasi ili kuweza kufunga.
Ni bao lake la tatu sasa katika mechi za watani wa jadi. Amefunga yote katika mechi za Ligi Kuu, tena mara tatu mfululizo. Kwa hivi karibuni ni Amissi Tambwe aliyeweza kufanya hivyo, wengine wameshindwa.
Nyoni kanoga huyo
Kuna Erasto Nyoni mmoja tu nchini. Anakaba, anamiliki mpira, anapiga krosi na pasi za mabao. Anacheza kwa kadri anavyojisikia. Kuna wakati anapiga chenga pia. Anajiamini mno.
Huyu ndiye Nyoni aliyeonwa na Marcio Maximo. Nyoni aliyedumu kwenye timu ya Taifa kwa miaka 11 sasa. Amekuwa msingi mkubwa katika mechi za Simba. Anafungua nafasi na kushambulia katika muda mwingi.
Krosi zake zimekwenda shule. Juzi Jumamosi alitoa pasi yake ya sita ya bao kwa msimu huu. Hakika Simba imenufaika zaidi ya usajili wake.
Okwi mfukoni
Huwa inatokea mara chache kwa mchezaji wa aina ya Emmanuel Okwi kuwekwa mfukoni. Alifanywa hivyo na beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’. Okwi alikuwa kama mtumishi hewa.
Hakuweza kukokota mpira wala kupiga chenga. Hakutengeneza mpira wowote wa hatari kwa Yanga. Ilikuwa ngumu kuamini kuwa ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu. Okwi anaweza kuwa hatari katika kufunga lakini sio katika mechi kubwa tena. Okwi wa sasa anakabika, sio kama yule wa miaka miwili nyuma.
Anaweza kuzifunga Ruvu Shooting na Njombe Mji, lakini kwa mechi kubwa tusubiri kwanza.
Tofauti na Okwi, Ibrahimu Ajibu alionekana hatari. Pengine kutokana na umri wake mdogo na kasi yake kubwa. Pengine kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira. Ajibu alijaribu kufanya kitu kwenye mchezo huo.
Licha ya kwamba hakufunga, bado Ajibu alionekana zaidi ya Okwi.
Mwamuzi alijaribiwa
Mwamuzi Elly Sasii alilipata joto la mechi ya watani. Mechi ya Ngao ya Jamii haikuwa na kasi kama ya juzi ambayo ilikuwa moto na iliyohitaji mwamuzi jasiri.
Sasii aliweza. Aliwaweka wachezaji wote chini ya himaya yake. Hakutaka kuharibu mchezo kwa kadi za mapema lakini baadaye mambo yalivyobadilika alizigawa. Hakutishwa na yeyote.
Aliamua kilichokuwa sahihi. Tukio kubwa pekee lililompita ni lile la Kelvin Yondani kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, ilikuwa kipindi cha kwanza. Bahati mbaya ama nzuri, Sasii hakuona. Tofauti na hapo alifanya vizuri.
Yanga imebadilika
Ukiachana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, Yanga iliyocheza mechi tatu za mwanzoni msimu huu na hii ya juzi ni tofauti. Wachezaji wake sasa wamechanganya. Kocha wa George Lwandamina, hakiika amefanya kazi kubwa. Yanga sasa inacheza soka la kasi na inashambulia.
No comments:
Post a Comment