SIKU zote maisha halisi huwa yapo ndani ya nyumba. Huenda wengi wetu wakawa hawaelewi, lakini ukweli ni kwamba kuna tofauti kubwa kati ya mtu unayekutana naye mtaani na akiwa nyumbani kwake, iwe na familia yake au peke yake.
Ndani ya nyumba, ndipo huishi maisha yake halisi, yasiyo na maigizo wala mbwembwe. Ni kuanzia hapa, ndipo unapoweza kupata A,B,C ya mtu kuhusu maisha yake ya nje. Unaweza kumkuta mtu mkali sana kazini, lakini kumbe nyumbani kwake ni mpole hadi anakera.
Wapo baadhi yetu ambao hulazimika kuwa vile tulivyo nje ya nyumba zetu kutokana na mazingira. Askari akiwa kambini anapokea maagizo ya bosi wake bila kuuliza swali kwa sababu ndiyo utaratibu, lakini huyohuyo akirejea mtaani hakubaliani na jambo lolote la kijamii pasipo kuhoji. Lakini hata hivyo, wapo watu ambao hawana tofauti ya maisha yao ya nje na ndani ya nyumba. Kama haambiliki nyumbani na hata nje yupo hivyohivyo na endapo ni mtu mnyenyekevu kazini na mtaani, basi hata familia yake inaelewa hivyo.
Nimeanza hivi kwa kuwa ninamlenga msanii wa muziki na filamu, Zuwena Mohamed au kama wengi wetu tunavyomfahamu kwa jina la Shilole.
Huyu ni mwanamuziki mkubwa kwa kiwango chetu na anasimama hapo alipo kama kioo halisi cha jamii. Maisha yake ya kimapenzi yana kokoto kidogo, kwa sababu historia yake inaonyesha amewahi kubakwa wakati wa ujana wake na pia ni mtu anayependa kujihusisha kimapenzi na vijana wa kiume wenye umri mdogo kuliko yeye. Alifanya hivyo kwa Nuh Mziwanda na sasa yupo na kijana mwingine anayejulikana kwa jina la Uchebe. Wakati ule akiwa na Nuh, kijana huyo ambaye naye ni msanii, alikuwa akimlalamikia kwamba ni mbabe, hajatulia na mapepe hivi, kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akimpiga pale alipokwenda kinyume naye. Juzikati, kijana wake wa sasa, Uchebe naye aliposti katika mtandao akitoa lawama ambazo ni wazi zinamlenga Shishi Baby, akisema ni mwanamke mapepe, mlaghai na ambaye hatambui thamani yake mbele ya jamii. Kwamba anatumia uwezo wake wa fedha kumnyanyasa na vitu vingine kama hivyo.
Katika mapenzi, malalamiko ya mtu dhidi ya mwenzake ni ya kawaida, lakini yanapotokea mara kwa mara, yakimhusisha huyohuyo, hujenga picha kuwa hiyo ndiyo staili yake ya maisha. Sina tatizo na Shilole katika kuamua aina ya wanaume anaotoka nao, kwa sababu hili ni jambo la kuamua, kwa vile wamevuka umri wa miaka 18, lakini visa vyake vinaonyesha ana kasoro katika namna alivyo katika maisha yake ya kimapenzi. Mwanamke kuwa na uwezo wa kifedha ni jambo la kujivunia sana kwa sababu siyo wanawake wote wanaweza kuwa hivyo, lakini kutumia uwezo huo kama fimbo ya kuwachapa wapenzi wake, siyo
jambo la busara.
Huenda hii ndiyo sababu ya wanawake wengi wenye vipato vikubwa kushindwa kutulia katika uhusiano wao, kwa sababu ya kufikiri fedha ndiyo kila kitu. Na kwa ishu ya Shilole, nadhani huenda ndiyo maana anaamua kuwachukua vijana wadogo ili aweze kuwadhibiti. Shishi, kuwa mwanamke hakukufanyi uwe mnyonge kwa mwanaume, lakini kwa mujibu wa tamaduni zetu, mwanamke ni mtu asiyetegemewa ampige mwenza wake, amnyanyase au hata kumdharau.
Kuna kitu Shilole anahitaji, hasa wataalam wa saikolojia, kwa sababu hata kitendo chake cha kuwahitaji vijana wadogo kiumri, ni tatizo, achilia mbali tabia hiyo ya kuwabutua. Lakini unajiuliza, kama mwanamke una fedha zako na umebarikiwa uwezo wa kuwarubuni vijana hadi wakavutika na wewe, kwa nini tena unawapiga na kuwanyanyasa? Maana unawatafuta mwenyewe, unawagharamia, kumbe tatizo ni nini tena? Kama vipi achana na hao wategemezi, tafuta wanaume wa umri wako uhangaike nao uone muziki wao!
No comments:
Post a Comment