Okwi apewa mechi tatu za mtego - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Tuesday 31 October 2017

Okwi apewa mechi tatu za mtego

KITENDO cha staa wa Yanga, Ibrahim Ajib kutamba katika mechi za ugenini kumeongeza mchecheto kwa hasimu wake, Emmanuel Okwi ambaye atalazimika kuibeba Simba katika mechi tatu zijazo za ugenini ingawa Kocha msomi, Mshindo Msolla ameonyesha wasiwasi.

Ajib amefunga mabao manne kwenye viwanja vya ugenini msimu huu na kuisaidia Yanga kukusanya alama 10 katika mechi nne za ugenini, huku Okwi akishindwa kufunga bao hata moja katika mechi mbili za ugenini alizocheza.

Kutokana na Okwi kuchemsha kwenye viwanja vya ugenini, Simba imekuwa na wakati mgumu kwenye viwanja hivyo ikikusanya alama tano tu katika mechi tatu ilizotoka nje ya Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ajib alifunga katika michezo dhidi ya Njombe, Kagera na Stand United huku akishindwa kufunga dhidi ya Majimaji pekee. Okwi alichemsha dhidi ya Mbao na Stand United huku akikaa benchi kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.

Ratiba inaonyesha kuwa, Simba itacheza michezo mitatu kati ya mitano ijayo ugenini, hivyo kumuweka Okwi katika wakati mgumu. Mechi hizo ni dhidi ya Mbeya City na Prisons huku pia wakisafiri kwenda Mtwara kucheza na Ndanda. Simba itakamilisha michezo hiyo kwa kucheza na Lipuli na Singida United nyumbani.

“Okwi wa sasa siye yule wa miaka ya nyuma. Umri umesogea na kasi yake imepungua. Hana uwezo wa kupunguza mabeki tena kama alivyokuwa akifanya, aina yake ya uchezaji imekuwa moja,” alisema kocha wa zamani wa Taifa Stars, Professa Mshindo Msolla.

“Anatakiwa kubadilika kidogo kwenye mechi hizo za ugenini. Unajua pia viwanja vya huko ni vigumu. Nadhani atakuwa na wakati mgumu kufunga, ufundi unakuwa kidogo,” alisema Msolla.

Wakati huo huo, Ajib naye atalazimika kufanya vizuri pia kwenye Uwanja wa Uhuru, kwani amefunga bao moja tu katika mechi nne walizocheza. Alifunga dhidi ya Ndanda na kuchemka dhidi ya Mtibwa, Lipuli na Simba. Ratiba ya mechi tano zijazo za Yanga ni ugenini dhidi ya Singida United na Mbao FC huku ikicheza nyumbani dhidi ya Prisons, Mbeya City na Mwadui.
“Yanga itakuwa na mechi ngumu pia. Mfano mchezo wa Mbao FC ambayo imekuwa ikiikamia. Timu ndogo huwa zinapenda kucheza vizuri mechi kubwa,” alisema Msolla.

Naye Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema msimu huu umekuwa mgumu kutokana na timu nyingi kujiandaa vema, lakini wanapambana kutetea taji lao.

No comments:

Post a Comment