MABINGWA wa Kombe la FA, Simba, leo wanashuka dimbani kucheza mchezo wao wa tatu wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga, katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Simba wanashikilia nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kucheza michezo miwili ambapo ilishinda mchezo wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting mabao 7-0 na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Azam.
Endapo Simba itashinda mchezo wa leo, itakalia kiti cha usukani kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi saba, lakini ikiwa na idadi kubwa ya mabao.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi anaongoza kwa mabao baada ya kufunga mabao manne katika mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting na kuifanya Simba kumaliza mchezo huo kwa ushindi wa mabao 7-0.
Mchezaji huyo huenda leo akaongeza idadi ya mabao yake kutokana na Kocha Joseph Omog katika mazoezi yake kuifanyia kazi safu yake ya ushambuliaji, ambayo amekuwa akiilalamikia kuwa haitimizi majukumu yake vizuri.
Wekundu hao wa Msimbazi wanahitaji ushindi katika mchezo huo, ili waweze kurudi kileleni mwa Ligi Kuu na kuwapita wapinzani wao, Yanga, ambao jana walibanwa mbavu na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Majimaji ya Songea.
Kutokana na ubora wa kikosi cha Simba msimu huu, wanalazimika kufanya vizuri katika michezo yao, ili kuzidi kuwaaminisha mashabiki wao kuwa wanaweza kuchukua ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu mitano mfululizo.
Na kutoka na hali hiyo, huenda kikosi cha Simba leo kikawa na utofauti na kile ambacho kimekuwa kikitumika katika michezo kadhaa ya nyuma, kutokana na mazoezi yaliyokuwa yakifanyika wiki nzima kujiandaa na mchezo huo.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema kuwa, timu yake ipo imara kwa ajili ya mchezo huo, na wameyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye timu yao wakati wa mchezo wao dhidi ya Azam FC na ana uhakika wa kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Khalid Adam, alisema wanatambua ugumu wa mchezo wao dhidi ya Simba, lakini watahakikisha wanapata ushindi wa pointi tatu bila kujali majina ya wachezaji wa kimataifa wanaokutana nao.
Aliongeza kuwa, lengo ni kuona wanafanya vyema kuanzia mechi za awali, ili baadaye waweze kujihakikishia nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa, kikosi chake kinakabiliwa na majeruhi watano, akiwamo Paul Nonga, Joram Mgeveke, Miraji Athuman, Antony Matogoro.
Mbali na mchezo huo, leo pia kutakuwa na mchezo mwingine dhidi ya Mbeya City na Njombe Mji.
Njombe Mji, ambao wamepanda daraja msimu huu, wana wakati mgumu kuhakikisha wanapata pointi katika mchezo huo, baada ya kupoteza michezo yote miwili waliyocheza.
TOA MAONI.
No comments:
Post a Comment