MIKAKATI YA SIMBA YAIACHA YANGA SOLEMBA. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Wednesday, 27 September 2017

MIKAKATI YA SIMBA YAIACHA YANGA SOLEMBA.

In Summary
 Inaonekana kuwa na mikakati kabambe ambayo imewaacha watani zao Yanga solemba.

VITA kubwa ya Simba na Yanga iko ndani ya uwanja, lakini nje ya uwanja pia hakuko salama.

Kuna ushindani mkali unaendelea baina ya timu hizo zenye mafanikio zaidi kwenye soka la Tanzania.

Simba na Yanga ndiyo timu zenye mashabiki wengi nchini, lakini swali kubwa limebaki juu ya namna ambavyo zimeweza kuwatumia mashabiki wao kama fursa ya kupata umaarufu na kipato.

Mbali na idadi hiyo kubwa ya mashabiki, bado kumekuwa na vita kubwa ya Simba na Yanga juu ya uwekezaji nje ya uwanja, Simba mpaka sasa ndiyo kinara.

Inaonekana kuwa na mikakati kabambe ambayo imewaacha watani zao Yanga solemba.

Makala haya yanakuletea namna ambavyo Simba imeweza kujiimarisha nje ya uwanja kuliko watani zao ambao kwa sasa wana ukata mkubwa wa kifedha.

Mitandao ya Kijamii
Fursa kubwa kwa Simba na Yanga sasa ni namna ya kuvuta mashabiki wengi kwenye mitandao yake ya kijamii kama Facebook, Instagram na Twiter ambayo ndiyo maarufu zaidi nchini.

Takwimu zinaonyesha Simba imefanikiwa kuvuta wafuasi wengi katika akaunti yake ya Facebook na Instagram kuliko watani zao Yanga ambao ndiyo klabu kongwe zaidi nchini.

Simba ina wafuasi 360,494 kwenye ukurasa wake wa Facebook huku watani zao Yanga wakifanikiwa kuvuta watu 205,607 tu mpaka sasa licha ya kufanya vizuri uwanjani na kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara.

Hii inamaanisha watu zaidi ya 150,000 wanaifuatialia zaidi Simba kwenye Facebook, inavutia sana.

Kwenye mtandao wa picha wa Instagram, Simba inakimbiza pia ikiwa na wafuasi 192,000 ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya wafuasi 79100 wa Yanga.

Huko Youtube
Licha ya kuwa Simba inakimbiza pia kwenye Youtube, bado namba ya watu waliojiunga na kupata video za timu hizo mbili kwenye mtandano huo wa video ni ndogo. Simba na Yanga zinadaiwa kuwa na mashabiki zaidi  ya 20 milioni nchini lakini wanaoifuatilia hawafiki hata 25,000.

Mpaka sasa ni watu 10,355 tu waliojiunga moja kwa moja kuona video za Simba kwenye Youtube yao, ikiwa ni idadi ndogo mno kulinganisha na idadi ya mashabiki wa timu hiyo ndani na nje ya nchi.

Yanga ndiyo ina hali mbaya zaidi kwani ni wafuasi 9,553 tu waliojiunga na Youtube yake huku video zake nyingi zikiwa zimetazamwa na watu 5,000 ama pungufu.
Simba, Yanga TV
Uwekezaji mwingine wa Simba na Yanga nje ya uwanja ni kuanzisha kipindi cha televisheni kupitia Azam TV. Vipindi hivyo vinafahamika kama Simba TV na Yanga TV.
Simba imeinyoosha Yanga kwenye kitengo hiki kwani ilisaini mkataba wa kuanzisha kipindi hicho mwaka 2013 na kila mwaka imekuwa ikichukua Sh100 milioni kutoka Azam TV.

Yanga ndiyo imesaini mkataba mwaka huu ambao unafanana na ule wa Simba na kwa mwaka itapa kiasi hicho hicho cha fedha.

Wakati Simba ikiwa imeshanufaika kwa miaka minne, Yanga ndiyo kwanza inasubiri kupata fedha hizo kwa mara ya kwanza.

Tovuti, APP
Yanga mpaka sasa bado haina tovuti (website) yake wala App inayota habari ramsi za klabu. Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten ndiyo kwanza anafanya kazi kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Kwa upande wa Simba ina tovuti yake inayotoa habari rasmi za klabu pamoja na App ambazo zote zipo chini ya Kampuni ya EAG Group. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mpaka sasa watu zaidi ya 120,000 wamepakua App ya Simba.

Vitega uchumi
Huku Simba ndiyo imenoga zaidi. Licha ya timu zote zina majengo eneo la Kariakoo, Dar es Salaam ni Simba tu inayonufaika kifedha.

Simba ina majengo mawili Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo na imeweka wapangaji ambao kwa mwaka wanalipa zaidi ya Sh350 milioni.

Yanga kwa upande wake inalitumia jengo lake lililopo kati ya Mitaa ya Jangwani na Twiga kama ofisi za klabu katika uendeshaji wa shughuli zake za kila siku.
Simba inaendesha pia biashara ya jezi kupitia Kampuni ya EAG Group ambayo kwa mwaka inawapatia fedha kimtindo. Yanga bado haina biashara yoyote.

No comments:

Post a Comment