Ajibu aliyejiunga na Yanga akitokea Simba kwenye dirisha la usajili la msimu huu, mpaka sasa ameisaidia timu hiyo kujikusanyia pointi nane kwenye michezo yao minne ya ligi kuu, huku yeye akifunga mabao mawili.
Ajibu na Raphael aliyetokea Mbeya City, wote wamejiunga na Yanga msimu huu na wamekuwa na uhakika wa kuanza ndani ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo kinachonolewa na kocha, George Lwandamina, raia wa Zambia.
Ajibu anayetumia jezi namba 10 ndani ya kikosi hicho, amesema kuwa Raphael anayecheza sambamba na Papy Kabamba Tshishimbi, raia wa Congo, kwenye eneo la kiungo la timu hiyo, amekuwa akionyesha uwezo wa juu katika kila mchezo wao jambo ambalo limekuwa likimfurahisha yeye na kumpa imani kuwa kiungo huyo ataibeba timu hiyo na kuipa ushindi kwenye kila mechi, lakini pia atakuwa msaada kwao kwenye suala la kutwaa ubingwa.
"Kwangu nimekuwa nikikoshwa na kiwango cha kiungo wetu, Raphael Daud, katika kila mchezo wetu na hata kwenye mechi iliyopita mbele ya Ndanda FC, alionyesha uwezo mkubwa na wa hali ya juu, nadhani kwa kupitia uwezo wake itakuwa rahisi sana kwetu kushinda kwenye kila mchezo na pia tunaweza kutwaa ubingwa kama atadumu muda mrefu bila kuumia,” alisema Ajibu ambaye mpaka sasa ameshafunga mabao mawili.
No comments:
Post a Comment