IMEKUWA jambo la kawaida kwa wasanii wengi wa nje ya nchi kuja na mbinu tofauti ili kuwateka mashabiki na kuuza kazi zao, miongoni mwa wasanii hao ni Yemi Alade wa Nigeria.
Yemi amekuwa na staili ya kipekee ya nywele zake kila linapokuja suala la kuachia video, amekuwa akizibadilisha rangi hadi muundo mara kwa mara na hii imekuwa ikifanya kuonekana wa kitofauti kwa mashabiki.
Mbali na Yemi kuna Chris Brown, Omarion, Tyga, Kanye West na wengine kibao ambao wamekuwa hawatabiriki kimuonekano ikitokea wanataka kufanya projekti mpya.
Kibongobongo suala hili halikuwa kivile lakini kwa miezi ya hivi karibuni tumeshuhudia wakali wengi wakianza kuonesha kubadili staili ya nywele ili kuendana na projekti zao. Showbiz linakuanikia baadhi ya wakali hao;
BEN POL:
Alianza kubadili nywele na kuwa zenye rangi ya brown mpauko, mashabiki wengi walishtuka kumuona hivyo na hata alipoulizwa hakuweka wazi ni kitu gani kilimfanya kuwa vile.
Yalisemwa mengi lakini mwisho wa siku akaamua kubadili tena muonekano ambapo aliweka rangi ya kijani iliyokolea. Wiki kadhaa mbele akaachia video ya ngoma yake ya Natuliza Boli ambapo ndani yake alionekana aking’aa na nywele hizo.
VEE MONEY:
Wakati Ben Pol akiendelea kuwa gumzo na nywele zake, siku kadhaa mbele, mkali mwingine, Vanessa Mdee ‘Vee Money’ naye aliibuka akiwa amebadili muonekano wa nywele zake.
Ishu hii ilikuja siku chache baada ya kuachia albamu yake mpya ya Money Mondays. Ishu hiyo ya nywele ilisababisha mashabiki wengi kumfuatilia na kumuongelea mitandaoni.
ALIKIBA:
Tangu ameingia kwenye muziki, Ali Saleh Kiba ‘Ali- Kiba’ haku-wahi kuon-ekana akiwa na muo-nekano wa rangi katika nywele zake.
Baada ya Ben Pol kisha Vee Money, Kiba ambaye ni mmoja wa viongozi wa lebo ya RockStar4000 naye alionekana akiwa na rangi nyekundu kichwani mwake.
Kiba alizua gumzo sana mitandaoni lakini baada ya wiki aliamua kuondoa rangi nywele hizo na kurudi kama zamani ambapo aliingia katika ndoa.
Ishu imekuja ‘kubumburuka’ kuwa, lengo la Kiba kubadili rangi zile ilikuwa sehemu ya projekti yake inayotikisa kwa sasa inayokwenda kwa jina la Mvumo wa Radi ambapo video yake ameonekana akiwa na nywele zilezile nyekundu.
DIMPOZ:
Wakati Kiba akiwa gumzo, picha nyingine zilizagaa zikimuonesha Dimpoz akiwa amebadili muonekano wa nywele zake na kuwa brown iliyokolea.
Baada ya picha hizo kusambaa akiwa ziarani nje ya nchi, picha nyingine zilimwagika zikimuonesha akiwa sambamba na Kiba pamoja na meneja wao, Seven. Baadaye Dimpoz alikuja kubadilisha rangi nywele hizo na kurudi kama zamani.
Hata hivyo imekuja kubainika kumbe ilikuwa ni projekti ya muda mfupi ya wimbo wake mpya aliomshirikisha msanii kutoka Nigeria, Seyi Shay unaojulikana kama Yanje ambapo kideo chake Dimpoz ameonekana aking’aa kichwani na nywele za brown.
HARMONIZE:
Unaweza kusema ni miongoni mwa wasanii wa kwanza kuanza kubadili rangi nywele. Mashabiki wengi hawakujua lengo la mkali huyu kubadili muonekano wa nywele zake na kuwa brown.
Nyuma ya pazia, muonekano huo ulikuwa kwa ajili ya projekti zake ambazo zilianzia kwenye Ngoma ya Shulala akimshirikisha Korede Bello wa Nigeria kisha DM Chick akimshirikisha Sarkodie wa Ghana na mwisho akamalizia na Kwa Ngwaru akimshirikisha bosi wake, Diamond Platnumz.
No comments:
Post a Comment