HIVI RUGE 'anawakoseaga' NINI..? - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Saturday, 5 May 2018

HIVI RUGE 'anawakoseaga' NINI..?

Lameck Ditto ‘Ditto’ alianza kusikika miaka 15 iliyopita kwenye ngoma ya Darubini Kali ya Afande Sele. Kama ni movie tunaweza kusema kwenye ting’a lile alicheza kama mtoto mbea. Mnoko. Kiherehere.
Yaani alikuwa anakoleza pale anapoishia kaka yake. “Arabuni utanyongwa” moja ya mstari maarufu zaidi. “Unanyoosha miguu wakati shuka ni fupi?” Uwepo wake ulinogesha na ubunifu ulikuwa wa kipekee.
Nani alishangaa Sele kuwa Mfalme wa Rhymes kwa pini lile? Nani aligomea ushindi ule? Labda Soggy Dogy. Ule wimbo ulikuwa kama “Dawa ya mba, fangasi, upele, mapunyee... sumu ya panya. Wakati ule tulimuita Dogo Ditto.
Yupo THT kwa sasa. Bila Ruge kumpokea na kuamua kuwa naye pale sijui Ditto angekuwa katika hali gani hivi sasa. Kaenda THT akitokea kundi la La Familia kwa Chid Benz (eti jamani?) baada ya kuachana na Afande Sele.
Nidhamu, uvumilivu na bidii imebadilisha kila kitu kwenye maisha yake. Anatoa ngoma kwa muda anaotaka. Video anayotaka. Hana stress za kupanga foleni studio na interview za kina B Dozen. Mungu ampe nini, matende?
Kuna watu wapo kwa ajili ya kukupa moyo kwenye maisha ya kipaji. Watakusifia kuwa unaweza, wewe ni mkali, lazima utoke. Jide kitu gani bana, hakuwezi hata kidogo. Yaani kila aina ya maneno ya faraja utapewa.
Hao huishia kukusifia tu kwenye vikao vya baa au popote. Watakupa bia mbili tatu ili uwaburudishe huku wakijinasibu kufahamiana na kila mdau wa sanaa nchini (Yahaya). Na kama msanii mwenyewe ni msichana watakwenda mbele zaidi.
Bia nyingi. Sifa nyingi. Tantalila nyingi na mwisho wa siku hata kama msanii huyo hana mvuto wowote au umri mdogo, akili ya pombe itafanya amuone kama Beyonce na mtu mzima mwenzake na kuishia kushea naye shuka kwenye ‘kigesti’ jirani na hiyo baa.
Huwa hawana muendelezo zaidi wa kumsaidia baada ya hapo. Msanii akubali kuwa kicheche chake au aishie kwenye ‘data base’ ya idadi ya mademu zake. Wako wengi wa hivi.
Haohao pia ndiyo wanaowatia ndimu kina Mwasiti ambao tayari wana majina. Kina Recho na wenzao kuwa wanatumiwa na wajanja huku wao wakifa masikini na vipaji vyao. Msanii mpumbavu anawasikiliza, anaachana na watu sahihi anaenda kusikojulikana anaishia kujifia na kipaji chake.
Kama hukumfahamu kabla huyo Linnah. Kama hukuwahi kuwaona kabla Barnaba na Nandy inakuaje leo useme kuwa wanatumiwa na wajanja baada ya kuwaona kwenye runinga na majukwaa ya Fiesta?
Na msanii inakuaje ukubali maneno ya shabiki tu kuwa unatumiwa, ambaye pia kakuona baada ya uwekezaji wa akili za watu wengine kwenye kipaji chako? Na wewe unaamini maneno yake na kumuona mtu sahihi kwako? Akili za kuambiwa...
Sasa kuna watu ambao wanamsikiliza msanii. Wanagundua kuwa kuna kipaji na namna gani watamtumia ili kipaji chake kigeuke kuwa mfereji wa pesa. Msanii apate na muwezeshaji huyo pia afaidike. Hao ndio akina Ruge.
Hawa huwezi kuwakuta baa wakimsifia msanii na kumnunulia bia, huku wakijinadi kufahamiana na wadau wa sanaa. Ila majina yao utayasikia kwa wasanii huko huko baa wakiwaongelea kwa mema na mabaya.
Akina Jide walikuwa na kipaji kabla ya uwepo wao kando ya Ruge. Lakini pesa zimejenga urafiki nao baada ya kuonyeshwa njia na akina Ruge. Ndivyo ilivyo kwa akina Ray C kabla ya kufunga ndoa na unga miaka kadhaa iliyopita.
Hawa Jide na Ray C walianza kama watangazaji pale Clouds kabla ya kujikita mazima kwenye muziki. Kuna hawa wanamuziki wengine wa kike ambao hawakupitia njia hiyo ambao ndio wengi kwa sasa.
Wanaanza kumsikia tu Ruge. Wanajipa matumaini na imani kuwa siku wakikutana naye basi maisha yao yatabadilika ghafla. ‘Of coz’ inatokea hivyo kweli kwa wenye vipaji sahihi kama akina Ruby, Nandy na wenzao.
Kabla ya kukutana na Ruge, wanatamani hata mahojiano tu na akina B Dozen, kupanda ngazi za maghorofani pale Mikocheni. Na zaidi huumia mno wakiwaona wenzao kwenye majukwaa ya Fiesta wakifiestika kiamazing.
Wanakuwa na hasira sana ya kupata umaarufu kabla ya mafanikio. Hapo akili ya pesa hutengwa na akili ya umaarufu, shida inakuwa kujulikana na wanakuwa tayari kwa lolote ili mradi wajulikane.
Lakini wakipewa nafasi kidogo tu majina yakiwa makubwa kuliko viatu alivyovaa, akianza kutazamwa zaidi sura na umbile lake kuliko kusikilizwa sauti yake yaani umaarufu ukiwa mkubwa kuliko wigi alilobandika kichwani. akili zinamruka ghafla.
Wakati shida yake kabla ilikuwa ni umaarufu sasa anaanza kuwaza utajiri wa ghafla. Ndinga kali. Pamba za maana na gheto la ukweli. Hapa neno subira huwa adui namba moja kwenye moyo wake kuliko shetani.
Na ndipo mishipa yake ya fahamu huwa karibu sana na maneno ya wapuuzi huko mitaani kuliko waliomfikisha pale alipo. Neno ‘unaibiwa’ linapewa kipaumbele kuliko hata sala kabla ya kula na kulala.
Pesa ya shoo anaanza kuona haitoshi kukidhi mavazi yake ya kistaa, kustarehe kila wikiendi na kutoka na mashost zake kula bata. Anaanza kuona hastahili maisha yale anataka maisha ya juu zaidi ya pale ili aishi kistaa kweli kweli. Hii ni kwa Bongo Movie pia.
Mwisho wa siku masikio yake yanatoa nafasi kwa mapedeshee. Maana ubwege wa pedeshee ni kumuona msichana maarufu ni bora zaidi. Wanatapanya pesa kama majuha ili mradi katoka kimapenzi na staa fulani.
Na mastaa wa kike pesa ndiyo kila kitu. Wanaanza kusikilizwa mapedeshee kuliko simu ya B Dozen kwenye XXL. Anaanza kujiona yuko juu kuliko kipindi cha Leo Tena. Yuko bize na maisha ya starehe.
Simu ya Soud Brown inageuka sumu kwake. Miezi miwili nyuma alitamani kuhojiwa na Shilawadu, leo anawaona wale masela wanafki, wanoko na wachawi wa maisha yake. Mabega yake yako juu juu kama kasombwa na mafuriko.
Macho ya watu. Sifa za mashabiki. Mitongozo ya mapedeshee, msanii anaanza kujiona ni zaidi ya Clouds. Ruge kitu gani? Nidhamu inaanza kutoweka taratibu kama nywele kwenye utosi wa Sallam, yule meneja wa Diamond.
Sasa nani wa kuendelea kuishi na msanii wa namna hiyo? Atawekwa kando atanyanyuliwa mwingine kwa sababu kwenye foleni ya kutoka kimuziki kuna wanamuziki wengi kuliko hawa unaowasikia hii leo.
Na kwa kuwa mapedeshee walimpendea umaarufu na sasa kuna maarufu wengine kibao, yeye ataanza kutengwa. Ataonekana makapi kishatumika sana. Hapo ndipo anapoanza kukumbuka shuka asubuhi. Nani wa kumpokea? Kutoka kutaka umaarufu. Baada ya umaarufu wa kutaka pesa nyingi na starehe. Baada ya vyote kuja na kupita na kubaki yuleyule kama mwanzoni mwisho wa siku anaanza kujenga upendo na neno, “Ruge ananibania.”
Ruby kabla ya kukutana na Ruge kila aliyemsikia kwenye studio nyingi mjini alisema huyu demu ni balaa. Ni zaidi ya fulani na fulani na fulani. Nakumbuka mimi baada ya kumsikia nilisema huyu mtoto ni zaidi ya Rose Muhando.
Kuna wakati baada ya Ruby kuzingua sana nikaanza kuhaha kumsaka Rose Muhando nimuombe radhi. Ingawa hata hajui kuwa kuna binti nilisema yeye ni zaidi yake. Pamoja na hayo pia naye Rose anahitaji makala zaidi ya haya.
Sisi wote tuliishia kumsifia kwa mdomo na sauti zetu. Hatukumshika mkono. Hatukumnyanyua zaidi ya kumfariji kwa maneno na sifa kibao. Na naamini kabla ya kutoka alisikika na watu wengi sana.
Lakini Ruge hakuishia kumsifia tu kama sisi alifanya Tanzania yote itambue uwepo wa kipaji hiki. Alimfungulia dunia na kuwa anachotaka. Mtoto wa kike akapitiliza mlango na kufanya tusichotaka.
Karukaruka huko kama kipepeo kwenye maua mwisho wa siku karudi palepale. Kuwa na kipaji ni jambo moja na kukisimamia kipaji chenyewe ni jambo lingine kubwa zaidi kuliko hata kipaji chenyewe.
Najua kuna mapimbi watasema yalishaisha nayaendeleza ya nini? Upuuzi kama huu hauwezi kuisha kindezindezi tu lazima tuweke kumbukumbu sawa ili kina Nandy wasifanye upuuzu kama huu.
Ukisikiliza mahojiano ya Ruby kwa sasa haweki wazi kabisa sababu za kugombana na Ruge. Kinachofurahisha ni kwamba wako poa hivi sasa. Subiri tuone kile kipaji halisi kwenye mwili wa Ruby.
Lakini hebu ngoja kwanza wewe, usitufanye mabwege mdogo wangu wacha nikuulize.... “Ruby hivi Ruge anawakoseaga nini?”

No comments:

Post a Comment