WACHUMI WATAJA MAMBO HAYA YA USHINDANI KATIKA UTANDAWAZI. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Wednesday 4 April 2018

WACHUMI WATAJA MAMBO HAYA YA USHINDANI KATIKA UTANDAWAZI.

Wachumi wametaja mambo saba yanayoweza kusaidia Taifa kuwa na ushindani katika mazingira ya utandawazi.
Mambo hayo ni udhibiti wa bidhaa feki zinazoingia nchini, uboreshaji mfumo wa elimu, ujuzi, uboreshaji wa miundombinu, kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza thamani katika mnyororo wa bidhaa.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 4, 2018 wakati wa ufunguzi wa warsha ya 23 ya utafiti chini ya Taasisi ya Utafiti ya Repoa.
Wadau katika warsha hiyo wameibua hoja hizo zilizokijikita kwenye misingi ya uzalishaji wenye tija na ushindani katikati ya mazingira ya utandawazi na masoko.
Mtoa mada mkuu, Pauline Mbala Elago ambaye ni Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Forodha la Kusini mwa Afrika (SACU) amesema Taifa linahitaji kuimarisha mazingira ya biashara na ubora wa bidhaa zinazotokana na wazalishaji wa ndani ili kukua katika ushindani wa masoko ya kimataifa.
Hata hivyo, Waziri wa Katiba na Sheria,  Profesa Palamagamba Kabudi amesema pamoja na changamoto zilizopo hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zinatia matumaini ya kuwezesha nguvu kazi na miundombinu.
Profesa Kabudi ambaye amemuwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema: “Taifa limetoka mbali, hilo wengi wanalifahamu, tumepitia vipindi vigumu katika kutukomboa kiuchumi  lakini Serikali kwa sasa imeanza kuchukua hatua  kuhakikisha namna gani Watanzania wanakuwa na uwezo, ujuzi wa kushiriki uchumi wa viwanda.”
Baadhi ya hatua alizotaja ni ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa, uwekezaji katika mradi wa umeme pamoja na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

No comments:

Post a Comment