TUZO ZA GABO NA WEMA ZIMEKUWA FUNDISHO KWA WENGINE - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Friday, 6 April 2018

TUZO ZA GABO NA WEMA ZIMEKUWA FUNDISHO KWA WENGINE

SIKU moja nikiwa ‘kijiweni’ maeneo ya nyumbani kwangu Sinza jijini Dar, ghafla ukaanza mjadala kuhusu Bongo Muvi. Mjadala huo ulikuja baada ya mmoja wa vijana ambaye ni msanii wa Bongo Fleva kudai kuwa, Bongo Muvi imekufa tangu Steven Kanumba afariki dunia.
Wapo walioonekana kumuunga mkono msanii huyo lakini kuna baadhi walionesha busara na kusema, si kwamba Kanumba kaondoka na Bongo Muvi yake kama baadhi wanavyodhani ila ukweli ni kwamba, waigizaji wazuri wapo, filamu nzuri zinatolewa kila siku lakini yapo mambo ambayo yanaonekana kuirudisha nyuma tasnia hiyo.

Kwa mfano wapo wasanii waliokuwa wakilalamika kwamba, kuna walioharibu soko la filamu zao kwa kuzidurufu kinyume na utararibu kisha kuziuza kwa bei chee. Unakuta filamu ilikuwa Part One iuzwe shilingi 3,000 na Part Two 3000, lakini unakuta pale Kariakoo na sehemu nyinginezo zenye watu wengi zinauzwa zote mbili kwa 2000. Wajanja wanapiga pesa, walioandaa filamu wanakufa njaa.
Lakini wapo wanaosema, channel za TV nazo zimeua soko la filamu na wengine kudai Series nazo ni chanzo. Kwa kifupi kuna kudodora kwa soko la filamu lakini kuna kitu kikifanyika, mambo yanaweza kuwa mazuri.

Wakati soko la filamu likisengenywa na walio wengi, bado wapo ambao wana imani na wasanii wetu na kuendelea kuthamini michango yao.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Azam Media kupitia Channel yao ya Sinema Zetu waliandaa tuzo walizozipa jina la Sinema Zetu International Film Festival (SZIFF). Waandaaji wa tuzo hizo waliweka vipengele mbalimbali lakini leo nitazungumzia vipengele viwili vya Muigizaji Bora wa Kike na Muigizaji Bora wa Kiume.

Kama ulifuatilia vizuri tukio la utoaji wa tuzo hizo pale Mlimani City jijini Dar, utakuwa umeona jinsi Miss Tanzania 2006, ambaye kwa sasa amejikita kwenye uigizaji, Wema Sepetu na msanii Salim Ahmed Issa ‘Gabo’ walivyoibuka kidedea.
Kwa kifupi ndiyo walioziteka tuzo hizo na kuwaacha wadau wakiwa na mitazamo tofauti. Wapo waliokubali wasanii hao kupewa tuzo hizo lakini kuna ambao waliona haikuwa sawa. Hiyo wala siyo ishu kwa sababu ingekuwa ni jambo la kushangaza kama watu wote wangeona kuwa wasanii hao walistahili kushinda.
Lakini sasa niseme tu kwamba, kuna kitu cha kujifunza sana kwa wasanii hawa kutwaa tuzo hizo.

KWA WEMA SEPETU
Huyu mdada nakumbuka aliwika sana kwenye filamu miaka ya nyuma, wengi wakaonesha kumkubali. Lakini mbali na kuigiza kwake, amekuwa ni mtu asiyeishiwa na matukio. Kila kukicha utasikia kitu kuhusu yeye. Maisha yake ya kimapenzi hasa na mastaa wengi imemfanya awe gumzo.
Hiyo imemsaidia kuwa maarufu sana kuwashinda waigizaji wengine wa kike Bongo. Ila sasa katika siku za hivi karibuni, mdada huyu amekuwa hana ile kasi ya uigizaji, amekuwa akidili na mambo mengine ikiwemo siasa, jambo ambalo kwenye ulimwengu wa filamu lilimfanya afifie.

Wakawa wanaendelea kuigiza wasanii kama vile Riyama, Uwoya, Shamsa na wengineo. Sasa wakati mchakato wa zile tuzo unaanza, kweli Wema hakuwa ‘on fire’ kivile lakini ikumbukwe tayari ana hazina yake ya kupendwa sana na watu, nyota yake inang’ara, kwa hiyo hata kama alikuwa kafifia ilikuwa ni rahisi sana wale walio nyuma yake kumpigia kura na kumfanya ashinde.

Sasa basi, wale ambao wanapinga Wema kupewa Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kike na Msanii Bora Chaguo la Watazamaji wakumbuke yeye ni kipenzi cha watu na wao ndiyo waliompa hiyo tuzo. Zaidi inatakiwa na wasanii wengine wajue kuwa, mbali na kufanya vizuri kazi zao, wanatakiwa kufanya ‘fitna’ za kuhakikisha wanakuwa hawakauki kwenye midomo ya watu na kwenye mitandao pia.
Kwa mfano, Wema na Riyama ukiwashindanisha leo ni vigumu kutarajia Riyama atashinda, hii ni kwa sababu hata kama Riyama amefanya kazi nyingi sana nzuri, bado anazidiwa na Wema linapokuja kwenye suala la umaarufu na kupendwa.

GABO ZAGAMBA
Mara baada ya Kanumba kufariki dunia, wengi walitarajia Vincent Kigosi ‘Ray’ achukue mikoba lakini haikuwa hivyo. Matokeo yake sasa wakaibuka wasanii kibao wa kiume waliojinasibu kuwa, wao ndiyo watavaa viatu vya Kanumba.
Wasani hao walikuwa ni akina Yusuf Mlela, Rammy Galis, Gabo, Duma na wengineo. Cha ajabu katika hao, ni Gabo tu aliyeonesha mapema kabisa kuwa ana kila sifa ya kumrithi Kanumba.

Na kweli jamaa kapambana sana, kaonesha kuwa ni muigizaji kweli na kazi zake zikawa zinaonekana. Zipo filamu nyingi alizocheza lakini hii ya hivi karibuni aliyoungana na Wema ya Heaven Sent ilikuwa bomba, matokeo yake juzi akang’ara kwa kupata tuzo 5 ambazo ni Best Film, Best Actor, Best Director, Best Screen Play na Best Orijinal Music.
Kwa hiyo kwa Gabo nimejifunza kwamba, ukidhamiria kitu na ukaweka jitihada za dhati, ukamtanguliza Mungu, ndoto zako zitakuwa kweli.

No comments:

Post a Comment