Mjadala huo umekuja kufuatia baadhi ya watu kuhoji uhalali wa Zari ambaye ni Mganda kupata dili hilo nchini wakati hapa nchini kuna mastaa wengi wenye sifa kama zake.
Miongoni mwa watu maarufu waliolalamikia hatua hiyo ni mwanadada Faiza Ally akisema amesikitishwa na kitendo hicho akihoji kwa nini hakupewa Mtanzania.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Faiza alihoji kwa nini kampuni zinawapa kipaumbele wageni na kuwaacha wazawa.
“Mastaa wote Watanzania, watu wote hamkuona hata mmoja anaye stahili kupata dili zaidi ya Zari ? Kwa nini tunawapa kipa umbele wageni tunajidharau sisi?” amehoji.
Maoni hayo ya Faiza yalizua mjadala mkali mtandaoni, mashabiki ambao wengine walimuunga mkono na wapo waliompinga huku wakimuuliza kama anaona anastahili kupewa ubalozi kutokana na namna anavyolibeba jina lake.
Wakati Faiza akilalamikia hilo, Shamsa Ford amesema mastaa wenyewe hawajiweki katika hadhi ya kupewa ubalozi wa bidhaa.
“Naona tu watu wanalalamika kwa nini ‘madili’ yanawapita mastaa wa Bongo na wageni ndio wanapata nafasi hiyo. Mimi nina mtazamo tofauti kabisa. Kabla ya kuanza kumtafuta mchawi ni nani ni bora kwanza tukajikagua wenyewe kwanza. Nina uhakika kila biashara ina taratibu zake na kila biashara inahitaji faida,” amesema Shamsa.
“Hakuna mfanyabiashara atakayekubali kumchukua staa wa Bongo kisa uzalendo tu halafu apate hasara. Tusipinge ukweli sisi wenyewe baadhi ya wasanii tumevunja uaminifu kwa wafanyabiashara wakubwa kutokana na matendo yetu. Suala sio kujulikana tu ila unajulikana vipi?.”
Mastaa wengine waliompongeza Zari ni washindi wa Miss Tanzania kwa miaka tofauti Millen Magese na Hoyce Temu.
No comments:
Post a Comment