SENETA WA MAREKANI AMHOJI BOSS WA FACEBOOK KUHUSU KUTUMIA KISWAHILI. - Erick Picson Media

Erick Picson Media

Mkali wa Matukio na Habari za Burudani

Breaking

Saturday, 14 April 2018

SENETA WA MAREKANI AMHOJI BOSS WA FACEBOOK KUHUSU KUTUMIA KISWAHILI.

Mdau wa Kiswahili, Profesa Safari Abdallah Safari amesema kauli ya dharau ya Seneta wa Republican, John Kennedy ya kumtaka ofisa mtendaji mkuu wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg asitumie Kiswahili bali Kiingereza ambacho kila raia wa Marekani anaweza kuielewa inapaswa kupuuzwa.
Mbali ya kauli ya Profesa Safari ambaye ni mwanasheria kitaaluma, habari kutoka Washington, Marekani zinaeleza kuwa seneta pia ameshutumiwa na maseneta wenzake.
Alishutumiwa wakati wa kikao cha kamati mbili za Bunge; ya sheria na ya biashara ziliposikiliza utetezi wa Zuckerberg juu ya shutuma zilizoelekezwa kwake kuhusu ukiukwaji wa sera ya faragha na udhibiti.
“Ninapendekeza kwamba urudi nyumbani ukaandike upya na uwaambie wanasheria wako unaowalipa dola za Marekani 1,200 (Sh2.7 milioni) kwa sasa, sikukosei heshima, ni wazuri lakini waambie kwamba unataka iandikwe kwa Kiingereza na si Kiswahili ili Mmarekani wa kawaida aweze kuelewa. Huo utakuwa mwanzo,” alisema Seneta Kennedy.
Katika mahojiano hayo, Seneta Kennedy alishutumiwa kwa namna alivyotumia neno “sio Kiswahili,” wengi wakidai ni mbaguzi. Licha ya maneno hayo ya hasira, Seneta Kennedy alikataa kuomba msamaha kwa kauli hiyo.
Seneta Kennedy, wakati wa mahojiano na mtangazaji wa CNN, Erin Burnett, alisema: “Hakukuwa na jambo la kuomba radhi. Nafikiri kila mmoja alielewa hoja ambayo nilijaribu kusisitiza.”
Maseneta wa Marekani walimbana Zuckerberg wakitaka aeleze jinsi kampuni yake ilivyokuwa ikitunza taarifa na siri za watumiaji wa mtandao wake.
Akizungumza kuhusu kauli ya seneta huyo, Profesa Safari alisema Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco), lilisema kuwa lugha zote duniani ni bora na hakuna inayozidi nyingine.
“Kwa hiyo kauli yake ya kuona Kiswahili hakifai ni ya kupuuzwa tu, binafsi naona ni ujinga kwa sababu hakuna utamaduni unaozidi utamaduni mwingine na tamaduni zote duniani ni sawa, hivyo lugha ni utamaduni,” alisema Profesa Safari.
Alisema lugha ya Kiswahili inapaswa kutumika mahali popote kama zilivyo nyingine nyingi duniani.

No comments:

Post a Comment