Moja ya vitu vinavyoleta hamasa katika sanaa ni tuzo. Kilio kilikuwapo kuwa watokee wadau wa kurudisha heshima ya tasnia ya filamu na sasa kimepata mkombozi ambao ni Azam Media walioamua kuja na tuzo za Sinema Zetu International Film Festival.
Kabla ya tuzo hizi kutolewa, filamu ilionekana si kitu tena, hata waigizaji wanaolalamika sasa wengi hawatoi filamu tena na wamekimbilia kwenye tamthilia.
Wadau wa filamu walibaki na wimbo mmoja tu, kwamba ili kulifufua soko anahitajika mtu mmoja wa kujitoa muhanga kuamsha tena ari ya Watanzania kuzipenda na kuzithamini.
Kwa namna ambayo wengi hawakuizungumzia ni tuzo. Huenda ni wachache sana walioamini kuwa kinachoweza kuamsha hamasa ya filamu nchini.
Ujio wa tuzo hizi ni kitu ambacho wasanii wa maigizo nchini wanatakiwa kukipokea kwa mikono miwili na kuwapongeza waandaaji kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Kulikuwa na kilio cha wasanii kutothaminiwa. Hakuna thamani ambayo mwigizaji au msanii yoyote anaweza kupewa kama kutuzwa.
Lakini kutuzwa kuna taratibu zake. Wapo wasanii wanaoamini wao ni bora lakini kwa kipimo gani? Wanajiita bora kwa kipimo gani, naani amewapima wao kujiona bora.
Kuna waigizaji wengi waliingia kwenye uigizaji kwa sababu ya mwonekano na skendo ambazo wasambazaji enzi hizo walipenda kwa sababu waliuza.
Uuzaji kazi mbovu kutoka kwa waigizaji wasio na vipaji ndio umelifikisha soko la filamu hapa.
Katika moja ya majibizano ya wasanii wiki hii kuna mmoja alimwambia mwenzake kuwa huu ni wakati wa wasanii kutuzwa kwa kazi zao na si kuuza haki.
Ukweli mchungu ni kwamba huu ni mwanzo mpya wa tasnia ya filamu na hawa wanaolalamika wakifanya mchezo itawatema. Wakibaki kulalamika tu bila kufanya kazi.
Mabadiliko yatatokea wakati huu, hivyo ni vyema wasanii wanaona ipo haja ya kubadilika kwa sababu uwezekano wa kuwaacha nyuma ni mkubwa.
Utamaduni wa kubebana kutokana na majina umezikwa rasmi. Filamu zilzioshinda katika tuzo hizo ni ishara tosha kuwa kitakachowabeba si majina yao bali hadithi, mpangilio na upigaji picha wa viwango vya kimataifa.
Wema Sepetu
Ushindi wa Wema Sepetu umekuwa kiini cha majibizano katika mitandao ya kijamii, lakini lipo la kujifunza katika hili.
Kwanza wakati wasanii wameikimbia tasnia ya filamu kwa kuwa wasambazaji waliachana nayo, yeye aliweka fedha kutengeneza na kuanza kuuza mtandaoni.
Kila mwigizaji alisema hawezi tengeneza filamu kwa sababu atapoteza fedha zake. Lakini Wema Sepetu na Gabo Zigamba kwa mapenzi ya tasnia hiyo walitengeneza filamu na kuziingiza sokoni na kuziuza kidijitali.
Mwigizaji Steve Nyerere alitaja orodha ya wasanii anaoona wanafaa kushinda katika tuzo hizo, lakini hakuvitaja walau hata kwa kutolea mfano wa mafanikio waliyoyapa huko nyuma.
Kwa mfano unaweza kusema mwigizaji fulani anastahili kupata tuzo kwa sababu filamu yake aliyotoa mwaka juzi (ukitaja kwa jina) imeuza nakala kadhaa, imeshinda tuzo kadhaa ndani na nje ya nchi.
Inawezekana kweli aliowataja ni waigizaji wazuri lakini wamefanya nini kinachoonekana? Je, si hao aliowataja wamekuwa anguko la tasnia iliyokuwa imeajiri watu wengi kuliko sanaa yoyote nchini?
Katika ushindi wa Wema Sepetu pia lipo la kujifunza kwani baada ya kutwaa tuzo, siku tatu baadaye akapata kampuni ya kusambaza filamu hiyo.
Hii ni ishara kuwa biashara ipo ila ilikuwa inasubiri kuchagizwa tu.
Muhimu
Ni kuaminini kuwa Tuzo za zimekuja kuamsha tasnia ya filamu nchini kwa kuwa wasanii wengi wanaolalamika sasa walishazikimbia na kuhamia kwenye tamthilia.
Nafasi ya kupata tuzo mwakani ipo muhimu ni kuandaa filamu zenye ubora kwa kuwa vigezo na masharti vinajulikana
Umuhimu wa tuzo hizi ni kufungua njia nyingine za kuistawisha tasnia ya filamu nchini.
No comments:
Post a Comment